Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kesi ya mkurugenzi wa IPTL yapewa muda majadiliano

338a38d7eacb8181dd8ba36c3f651a2f Kesi ya mkurugenzi wa IPTL yapewa muda majadiliano

Fri, 11 Jun 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mkoani Dar es Salaam imekubali kutoa muda kwa pande mbili katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Mkurugenzi wa Kampuni ya Kufua Umeme ya IPTL, Habinder Seth kufanya majadiliano kutokana na maombi yaliyotolewa na mshtakiwa huyo.

Hayo yalitokea jana kesi hiyo ilipotajwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaid baada ya Wakili wa Serikali Mkuu, Martenus Marandu kuomba mahakama iwape muda wa kukutana na kufanya mazungumzo na Seth.

"Mheshimiwa! Mshtakiwa aliandika barua kupitia wakili wake na sisi Jamhuri tukaona ni vema tuje mbele zako kuomba tukutane na mshtakiwa kwa ajili ya kupata ufafanuzi wa kile ambacho amedhamiria kuomba kukifanya, na ikiwa upande wa utetezi hauna pingamizi na ombi letu tunaomba ikikupendeza mahakama itupangie siku ya kesho (leo) ili tuweze kuleta mrejesho wa kile ambacho tutakuwa tumezungumza," alisema Marandu.

Hakimu Shahid alikubaliana na ombi la upande wa Jamhuri na kuahirisha kesi hiyo ambayo inatajwa tena leo.

Awali ilidaiwa kuwa, Seth aliandika barua ya maombi ya kumaliza kesi hiyo kwa njia ya makubaliano na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), lakini hatua hiyo ilikuwa inasubiri mwongozo wa mkurugenzi mpya wa mashtaka.

Hata hivyo baadaye Mei 6, 2021, Seth na mshtakiwa mwingine Joseph Makandege, waliwasilisha ombi lingine la kuondoa nia ya kufanya makubaliano na DPP kwa kile walichokidai kuwa mazungumzo hayo yalichukua muda mrefu kukamilika.

Mbali na Seth na Makandege mshtakiwa mwingine ni mfanyabiashara, James Rugemalira.

Washtakiwa Seth na Rugemarila wanakabiliwa na mashtaka 12 yakiwemo kula njama, kujihusisha mtandao wa uhalifu, kughushi, kutoa nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, kutakatisha fedha na kusababisha hasara ya Dola za Marekani 22,198,544.60 na Sh 309,461,300,158.27.

Washtakiwa wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Oktoba 18, 2011 na Machi 19, 2014 jijini Dar es Salaam pamoja na nchi za Afrika Kusini, Kenya na India.

Kwa upande wake, Makandege anakabiliwa na mashtaka matano likiwemo la kuisababishia Serikali hasara ya Dola za Marekani 980,000.

Chanzo: www.habarileo.co.tz