Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kesi ya mjane wa Bilionea Msuya hukumu yanukia

Miriam Mrita Msuya Kesi ya mjane wa Bilionea Msuya hukumu yanukia

Mon, 11 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imefunga rasmi usikilizwaji wa ushahidi wa kesi ya mauaji inayomkabili mjane wa aliyekuwa mfanyabiashara wa madini mkoani Arusha, Erasto Msuya, maarufu kama Bilionea Msuya; Miriam Steven Mrita na mwenzeke Revocatus Muyella, maarufu kama Ray.

Mahakama hiyo umefunga usikilizwaji wa ushahidi huo leo Ijumaa, Novemba 10, 2023, baada ya kukamilisha kupokea ushahidi wa pande zote, yaani ushahidi wa upande wa mashtaka na utetezi wa washtakiwa wenyewe pamoja na mashahidi wao.

Miriam ambaye ni mjane wa Bilionea Msuya, aliyeuawa kwa kupigwa risasi eneo la Mijohoroni, wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro, Agosti 7, 2013 na mwenzake Muyella, wanakabiliwa na shtaka moja la mauaji, wakidaiwa kumuua, Aneth Elisaria Msuya, aliyekuwa wifi yake Miriam.

Aneth ambaye alikuwa mdogo wake Bilionea Msuya aliuawa Mei 26, 2016 kwa kuchinjwa nyumbani kwake Kibada, Kigamboni, wilayani Temeke (wakati huo), jijini Dar es Salaam. Kesi hiyo ya jinai namba 103 ya mwaka 2018, inasikilizwa na Jaji Edwin Kakolaki.

Usikilizwaji wa ushahidi wa pande zote katika kesi hiyo umehitimishwa leo baada ya mshtakiwa wa pili, Muyella ambaye ni shahidi wa tano wa utetezi katikia kesi hiyo kufunga utetezi wake akitumia siku mbili.

Miriama ambaye ndiye mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo, ndiye aliyefungua pazia la utetezi.

Miriam alifunga utetezi wake baada ya kuita jumla ya mashahidi wanne, akiwemo yeye mwenyewe na mashahidi huru watatu, huku akitumia jumla ya siku tisa, yeye mwenyewe akisimama kizimbani kwa siku sita na mashahidi wake hao watatu wote kwa pamoja wakitumia siku tatu.

Muyella amehitimisha utetezi wake baada ya kuulizwa maswali ya dodoso kutoka kwa mwendesha mashtaka Wakili wa Serikali, kuhusiana na ushahidi wake wa msingi, pamoja na maswali ya kusawazisha kutoka kwa wakili wake, Nehemiah Nkoko, kufafanua baadhi ya hoja zilizoibuliwa katika maswali ya dodoso.

Awali, katika ushahidi wake wa msingi, Muyella ambaye alijitambulisha kuwa alikuwa mjumbe wa Kamati ya Siasa na Uchumi wa Umoja wa Vinaja wa Chama cha Mapinduzi (CCM – UVCCM) mkoa wa Arusha pamoja na mambo mengine alikana kuhusika na mauaji hayo.

Akiongozwa na wakili wake, Nkoko, Muyella alikana kuwepo eneo la tukio kwa tarehe zinazotajwa na upande wa mashtaka, akidai kuwa kwa tarehe hizo zote alikuwa Arusha akishughulika na mkewe ambaye alikuwa amejifungua watoto pacha.

Pia alikana majina yake yanayosomeka kwenye hati ya mashtaka kuwa si yake.

Katika hati ya mashtaka, mshtakiwa huyo ametajwa kama Revocatus Everist Muyella, lakini yeye adai kuwa majina yake halisi ambayo amekuwa akiyatumia siku zote kama yanavyosomekam katika cheti chake cha kuzaliwa na hati yake ya kusafiria ni manne ambayo ni Revocatus Everest Patick Muyella.

Alidai kuwa alipokamatwa Agosti 19, 2023, akiwa ofisi za UVCCM, kisha kesho yake akasafirishwa kupelekwa jijini Dar es Salaam, alipoelezwa tuhuma zake alikana na kwamba hata simu zake zikichunguzwa mawasiliano na ndugu zake na miamala ya fedha zingethibitisha kuwa tarehe hizo alikuwa Arusha.

Pia alidai kuwa hakuwahi kupekuliwa nyumbani kwake bali alipekuliwa katika kituo cha Polisi, huku akirejea hata hati ya Polisi ya upekuzi iliyowasilishwa mahakamani kama kielelezo cha upande wa mashataka inaonesha kuwa aliyepekuliwa ni Revocatus P. Molel na siyo yeye.

Vilevile alikana madai ya upande wa mashtaka ya kwenda Kigamboni kupanga mipango ya mauaji (akiwa na Miriam), Mei 15, 18, 20, 23 na tarehe ya tukio la mauaji Mei 25, 2016.

Badala yake alidai kuwa hakuwahi kufika mkoa wa Dar es Salaam na wala Kigamboni hajawahi kufaika, kwani siku zote hizo alikuwa Arusha.

Alibainisha kuwa uthibitisho ni kwamba simu ni mawasiliano ya kieletroniki, ujumbe mfupi wa maneno, minara kiujumla mawasiliano haya yangeonyesha kama nahusishwa na mshtakiwa wa kwanza hakuna shahidi aliyeithibitishia mahakama kama tarehe hizo alikuwepo Dar es Salaam.

Muyella pia alikana kuwa hajawahi kuchukuliwa sampuli ya mpanguso wa mate yake kwa ajili ya kupima vinasaba kama inavyodaiwa kuwa vinasaba kutoka katika mpanguso wa mate yake vilifana na vile vilivyokutwa kwenye kisu kianchodaiwa kutumika katika mauaji hayo.

Baada ya ushahidi wake huo mkuu ndipo alipohojiwa maswali ya dodoso. Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano hayo baina ya wakili wa Serikali, Paul Kimweri na shahidi (mshtakiwa huyo) pamoja na wakili wa utetezi, Nkoko na mshtakiwa.

Wakili Kimweri: Umeieleza mahakama kwamba tarehe 15/5/2016 ulikuwa Arusha sababu mkeo alikuwa amejifungua, ieleze Mahakama alilifungua tarehe ipi?

Shahidi: Usiku wa tarehe 12 kuelekea 13, mwezi wa Tano.

Wakili: Utakubaliana nami sas kwamba kati ya tarehe 15/5/2016 (tarehe wanayodaiwa kwenda Kigamboni kwa marehemu Aneth kwa mara ya kwanza) mpaka 25/5/2016 (siku ya tukio la mauaji ya Aneth) mkeo tayari alikuwa ameshajifungua?

Shahidi: Ni sawa

Wakili: Lakini ukiachilia mbali hilo, inawezekana mtu ukawa safarini mke akajifungua au haiwezekani ukawa safarini mkeo akajifungua?

Shahidi: Inawezekana.

Wakili: Ukichilia mbali maneno tu uliyoyasema una ushahidi wowote wa nyaraka wa kujifungua mkeo, cheti cha kuzaliwa nk?

Shahidi: Vikihitajika vipo na nilishatoa maelezo yangu kwamba kwenye simu zangu kuna ushahidi wote lakini hapa mahakamani hakuna.

Wakili: Hizi simu ambazo unasema ndizo utategemea zioneshe kuwa hukuwepo eneo la tukio, utakubaliana na mimi kwamba simu ni kitu ambacho kinabebeka au unaweza ukakiacha?

Shahidi: Ni sawa

Wakili: Kwa sababu hiyo ukiziacha simu Arusha wewe ukaenda sehemu nyingine watu wa mtandao wakizitafuta wataziona ziko Arusha siyo?

Shahidi: Ni kweli

Wakili: Kuna maelezo umeyatoa hapa mahakamani kwamba aliyesaini na aliyefanyiwa hilo gwaride la utambuzi ni Revocatus Everist, siyo?

Shahidi: Nido

Wakili: Sasa wakati shahidi wa 12, Insp. Herry anatoa maelezo ya hilo gwaride hapa mahakamani, alikuelekeza wewe, ni sahihi?

Shahidi: Alini-point ndio sikatai

Wakili: Hata shahidi mwingine aliyekuja kuizungumzia gwaride la utambuzi, PW20, Nassib hata yeye alisema anaku-point wewe ukiachia mbali spelling za majina haya?

Shahidi: Alini-point, hata Mahakama inaona maana shtaka hili kuna jinisia ya kike na ya kiume na jinsia ya kiume ni mimi tu.

Wakili: Wakati huyu shahidi wa 12 anaomba kukitoa kielelezo hiki hizi hoja ulizitoa za kukipinga kutokana na majina na saini hazikuibuliwa ni kweli?

Shahidi: Ni kweli

Wakili: Wakili wako pia alikuongoza katika vielelezo PE8 (fomu ya gwaride la utambuzi) na DE13 (hati yake ya kusafiria) kuhusu saini zako ukasema hazifanani, wewe ni mtaalamu wa maandishi?

Shahidi: Mimi si mtaalamu wa maandishi.

Wakili: Kwa hiyo hoja za utaalamu wa maandishi kuhusu saini wewe huwezi kuzielezea?

Shahidi: Siwezi kuzielezea.

Wakili: Umeieleza mahakama kuwa tangu Agosti 19 ulipokamatwa hakuna upelelezi wowote uliofanyika dhidi yako na ulikataa pia kuchukuliwa sampuli za mate, aliyekamatwa kuhusiana na kesi hii utakubaliana nami kwamba ni wewe na si mtu mwingine?

Shahidi: Katika kesi hii, ehee ni mimi.

Wakili: Utakubaliana nami kwamba mashahidi wote walipozungumza hoja ya kuchukua sampuli mtu waliyem-point (waliyemuelekezea) ni wewe?

Shahidi: Ni kweli

Wakili: Segumba (Shahidi wa 15, aliyefanya uchunguzi wa vinadaba) wewe ulikuwa hufahamiani naye kabla ya tukio hili na ni kweli kwamba hajawahi kuwa na uhasama na wewe?

Shahidi: Sahihi.

Wakili: Ulisema jana kwamba uliomba simu zako (akiwa mahabusu), uliomba kwa maandishi?

Shahidi: Hapana

Wakili: Ulipokuja hapa mahakamani uliwahi kumuomba jaji kwa maandishi kwamba unaziomba?

Shahidi: Hapana, kuna hiyo notice of alibi (taarifa ya utetezi wa kutokuwepo eneo la tukio) tu.

Wakili: Ulieleza mahakamamkuwa pamoja na DNA ilibidi kuwe na uchinguzi wa damu ya Aneth isome kwamba ni ya Aneth, ni sawa?

Shahidi: Vielelezo vyote visome kwamba ni vya Aneth na siyo kudhaniwa.

Wakili: Lakini hakuna ubishi kwamba yule aliyekufa ni Aneth?

Shahidi: Yule alikuwa ni jinsia ya kike, najua tunashtakiwa kwa kituhumiwa kumuua Aneth Msuya.

Wakili: Kwa hiyo siyo kweli kwamba Aneth amefariki?

Shahidi: Ndivyo inavyosomeka kwenye document.

Wakili: Kwa hiyo ubishi ni kwamba nani alimuua Aneth?

Shahidi: Ndio

Wakili: Tunakubaliana kwamba Segumba akifanyia uchunguzi kisu hicho kilichomuua Aneth?

Shahidi: Mimi sikuwepo siwezi kujua.

Wakili: Lakini tunakubaliana kuwa ni kisu kinachodhaniwa kumuua Aneth?

Shahidi: Ndio kinachodhaniwa.

Wakili: Ulisikia Segumba akisema kuwa sampuli alizozifanyia uchunguzi zinafanana na vinasaba vya mtu anaitwa Revocatus Muyella?

Shahidi: Ni uchunguzi wake huo.

Maswali ya ufafanuzi kutoka kwa wakili Nkoko

Wakili: Shahidi hii ripoti ya DNA ina uhusiano gani na wewe?

Shahidi: Mheshimiwa Jaji kama nilivyosema awali mimi sikutolewa vipimo vya huo mpanguso wa mate.

Wakili: Uliulizwa kwa nini hukuleta maandishi kuomba simu zako ila kwenye notisi ya alibi kwa kumbukumbu zako hiyo ‘notice of alibi’ ulikuwa unamuomba nani?

Shahidi: Kwa maelekezo ya wakili wake anasoma para ya pili ya taarifa hiyo, ambayo imetaja simu zake kuwa ndizo atakazozitegemea katika utetezi wake wa kutokuwepo eneo la tukio na kwamba ziko katika miliki ya upande wa mashtaka.

Wakili: Vilevile ulisumbuliwa tarehe ya kujifungua mkeo, ukaulizwa inawezekana ukawa umesafiri tarehe 15 ukasema ndio, katika tarehe hizo utakubaliana na mimi inawezekana vilevile mtu mkewe akawa amejifungua akawa eneo lilelile?

Shahidi: Inawezekana.

Wakili: Uliulizwa kuhusu kutambuliwa na mashahidi mbalimbali ukasema wamekutambua sababu mshtakiwa wa kiume ni mmoja tu kwa nini umesema hivyo?

Shahidi: Nilisema hivyo kwa sababu mshtakiwa wa kiume ni mimi tu lakini wangekuwa wengi ndio ingekuwa kwa nini wewe kati ya hawa wengi?

Wakili: Uliulizwa kuhusu saini ( kwenye hati ya upekuzi na kwenye hati yake ya kusafiria) kama wewe ni mtaalamu wa maandishi ukasema siyo uliwezaje kufanya ulinganifu?

Shahidi: Kwa sababu ya kwangu iko kwenye passport.

Wakili: Uliulizwa kuhusu kisu vinasaba kwenye kinachodaiwa kutumika katika mauaji kuwa vinafafana na vinasaba vyako, unaielezaje mahakama?

Shahidi: Mheshimiwa jaji kilelezo cha kisu kusema kilipimwa kina DNA yangu mimi napinga tangu mwanzo sikupimwa, hata mwili (wa marehemu) haukupimwa vielelezo vilipimwa vyenyewe kwa vyenyewe.

Baada ya maswali hayo wakili Nkoko ameieleza mahakama kuwa wanafunga kesi (utetezi) upande wa mshtakiwa wa pili (Muyella) na Wakili Kimweri akaomba muda wa majuma mawili kuwasilisha majumuisho ya hoja, ambayo imeungwa mkono na mawakili wa utetezi, Kibatala na Nkoko.

“Basi kufuatia kukamilika kwa ushahidi wa pande zote mbili na maombi yaliyoletwa pande zote mbili zinapewa wiki mbili kuwasilisha majumuisho ya hoja ambapo zitatakiwa kuziwasilisha kabla au Novemba 27, 2023”, amesema Jaji Kakolaki.

Katika hoja hizo, mawakili wa pande zote watakuwa na kibarua cha kuishawishi mahakama ikubaliane nao.

Wakati mawakili wa Serikali watakuwa na jukumu la kuishawishi mahakama kuwa kwa mujibu wa ushahidi wake wameweza kuthibitisha bila kuacha mashaka kwamba washtakiwa wana hatia, mawakili wa utetezi kwa upande wao watakuwa na kibarua kuishawishi mahakama kuwa upande wa mashatka umeshindwa kuthibitisha shtaka bila kuacha mashaka.

Hivyo watakuwa na jukumu la kuchambua udhaifu wa ushahidi huo na namna ambavyo utetezi wa washtakiwa umeweza kuutikisa ushahidi wa upande wa mashtaka kiasi cha kuuacha na matobomatobo kiasi cha kutoweza kuwatia hatiani.

Baada ya hapo sasa hatima ya washtakiwa hao itabakia kwa mahakama katika uamuzi wake.

Jaji Kakolaki ameahirisha kesi hiyo mpaka Desemba 4 mwaka huu itakapotajwa kwa ajili ya kuangalia taratibu nyingine.

Siku hiyo inawezekana Mahakama ikafanya muhtasari wa ushahidi na baada ya muhtasari huo itatoa nafasi kwa wazee wa baraza kutoa ushauri wao kulingana na ushahidi kama washtakiwa wana hatia au hawana hatia, kisha mahakama itapanga tarehe ya kutoa hukumu

Chanzo: www.tanzaniaweb.live