Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kesi ya meneja wa zamani Benki ya Wanawake yapigwa kalenda

35556 Pic+kesi Kesi ya meneja wa zamani Benki ya Wanawake yapigwa kalenda

Thu, 10 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Upelelezi wa kesi inayomkabili aliyekuwa meneja wa Benki ya Wanawake Tanzania (TWB) tawi la Mkwepu, Priscus Shirima (37) haujakamilika.

Shirima ambaye ni mfanyabiashara na mkazi wa Dodoma Area D anakabiliwa na mashtaka matatu ikiwemo kufanya miamala ya uongo akiwa mtumishi wa benki hiyo, wizi na kutakatisha fedha kiasi cha Sh120 milioni.

Mwanasheria wa Serikali mwandamizi, Patrick Mwita ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Jumatano Januari 9, 2019 kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Mwita ameeleza hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Salum Ally wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Ally ameahirisha kesi hiyo hadi Januari 23, 2019  kesi hiyo itakapotajwa tena.

Katika shtaka la kwanza la kufanya muamala wa uongo akiwa ofisa wa benki, Shirima anadaiwa kuwa Juni 20, 2016 akiwa na nia uovu alifanya muamala wa uongo kwa kuhamisha Sh120 milioni kutoka akaunti namba 0310137001 ya Florah Lyatuu kwenda akaunti yake namba 0380073121.

Katika shtaka la pili la wizi akiwa mtumishi, Shirima anadaiwa siku na eneo hilo aliiba Sh120 milioni.

Shtaka la tatu ambalo ni utakatishaji fedha, mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Juni 2016 katika benki hiyo.

Anadaiwa alijihusisha na muamala wa Sh120milioni kwa kuruhusu na kufanya malipo kutoka akaunti namba 0380073121 inayomilikiwa na shirika, akilipa kampuni ya Sekorizi Ltd kupitia hundi tatu zenye namba 000127, 648806 na 1648791 huku akifahamu kuwa fedha hizo si halali.



Chanzo: mwananchi.co.tz