Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kesi ya mauaji ya Asimwe; marufuku kutaja majina ya mashahidi

Kesi Ya Mauaji Ya Asimwe; Marufuku Kutaja Majina Ya Mashahidi.png Kesi ya mauaji ya Asimwe; marufuku kutaja majina ya mashahidi

Thu, 22 Aug 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Bukoba imelikubali ombi la Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) la kuzuia kutumika kwa majina na taarifa za mashahidi katika kesi ya mauaji ya mtoto mwenye ualbino, Asimwe Novath.

Uamuzi huo wa Mahakama unatokana na maombi ya DPP kupitia maombi ya jinai namba 23143 ya 2024 ambayo yalisikilizwa chemba ili kulinda usalama wa mashahidi na ndugu zao, kwani kumekuwa na tishio la kiusalama dhidi yao.

DPP katika maombi hayo, ameeleza kumekuwepo na majaribio mbalimbali kutoka kwa washirika wa washitakiwa kupata majina na utambulisho wa watu ambao wanaweza kuwa mashahidi, kwa lengo la kuwadhuru ili wasitoe ushahidi wao.

Wajibu maombi katika maombi hayo ni Padri Elipidius Rwegashora, Novat Venant ambaye ni baba wa marehemu, Nurdin Ahamada, Ramadhan Jadius, Rwenyagira Burukadi, Danstan Burchad, Faswiu Athman, Gozbert Arikadin na Desdery Everigist.

Katika uamuzi wake alioutoa jana Jumatano Agosti 21, 2024, Jaji Gabriel Malata amezuia matumizi ya nyaraka ambazo zinaweza kutoa utambulisho wa mashahidi na nyaraka hizo, zitafanywa siri katika hatua zote za usikilizwaji wa shauri hilo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live