Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kesi ya kutekwa Mo Dewji, upande wa utetezi watoa ombi

85906 Pic+mo Kesi ya kutekwa Mo Dewji, upande wa utetezi watoa ombi

Wed, 27 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Upande wa utetezi wameuomba upande wa mashtaka kuharakisha upelelezi katika kesi ya kutekwa kwa Mfanyabiashara Mohammed Dewji 'Mo' ili kesi hiyo ifike kwenye hatua ya usikilizwaji.

Wakili wa utetezi, Maufudhi Mbagwa amedai hayo leo Jumatatu Novemba 25, 2019 mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam baada ya Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon kudai upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika.

Mbagwa amedai pamoja na maelezo ya upelelezi kuendelea hivyo tunawaomba upande wa Jamhuri wafanye haraka kukamilisha shauri hilo ili shauri hilo lifike kwenye hatua ya kusikilizwa.

"Mshtakiwa amekaa ndani muda mrefu tunaomba waharakishe upelelezi ili shauri liweze kuendelea mbele," amedai Mbagwa.

Baada ya maelezo hayo, Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi ameahirisha shauri hilo hadi Desemba 10, 2019 itakapokuja kwa ajili ya kutajwa.

Awali, mahakama hiyo ilitoa hati ya kuwakamata washitakiwa hao ambao ni Henrique Simbine, Daniel Manchice, Issac Tomo na Zacarious Junior wote raia wa Msumbiji na Phila Tshabalala ambaye ni raia wa Afrika Kusini.

Mmoja wa washtakiwa hao ambaye ameshafikishwa mahakamani hapo ni dereva wa taksi , mkazi wa Tegeta Mousa Twaleb.

Katika kesi hiyo inadaiwa Mei Mosi na Oktoba 10, 2018, katika maeneo ya jiji la Dar es Salaam na Johannesburg Afrika Kusini, kwa makusudi washitakiwa wote kwa pamoja waliendesha genge la uhalifu.

Pia, inadaiwa Oktoba 11, 2018 maeneo Hoteli ya Colloseum wilayani Kinondoni Dar es Salaam, Twaleb pamoja na watu wengine ambao hawapo mahakamani, walimteka nyara Mo kwa nia ya kumuhifadhi kwa siri na kumuweka maeneo ambayo ni hatari.

Pia, inadaiwa Julai 10, 2018 maeneo ya Mbezi Beach wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, Twaleb alitakatisha fedha ambazo ni Sh8 milioni wakati akijua fedha hizo ni kosa la kushiriki genge la uhalifu na makosa ya kupanga.

Mo alitekwa nyara Oktoba 11, 2018 alfajiri maeneo ya Hoteli ya Colloseum wakati akienda kufanya mazoezi na alipatikana Oktoba 20, 2018 katika eneo la Gymkhana.

Chanzo: mwananchi.co.tz