Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeshindwa kuendelea baada ya shahidi aliyetakiwa kumalizia kutoa ushahidi anauguliiwa na mama yake mzazi katika kesi inayomkabili mfanyabiashara, Papetua Gondwe kwa kujipatia kwa njia ya udanganyifu kiasi cha Sh312 milioni.
Wakili wa Serikali, Ashura Mzava alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu, Richard Kabate kuwa shauri hilo lilikuja kwa ajili ya kumalizia kutoa ushahidi lakini shahidi aliyekuwa wakimtegemea anauguliwa na mama yake mzazi ambaye amelazwa.
"Tunaiomba mahakama hii ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kuendelea na ushahidi, shahidi aliyetakiwa kumalizia ushahidi wake anauguliiwa na mama yake mzazi amelazwa hospitali ndiye anamuugaza hivyo anamsubiria mtoto wake anatoka mkoani Arusha ili aweze kukaa naye," alidai Mzava.
Baada ya maelezo hayo Hakimu Kabate aliahirisha shauri hilo hadi Februari 27, 2023 kwa ajili ya kuendelea na ushahidi.
Inadaiwa kiwa kati ya Aprili 22, 2019 ndani ya Mkoa na Jiji la Dar es Salaam kwa njia ya kudamganya, mshitakiwa huyo alijipatia kiasi cha Sh312,429,000 kwa njia ya udanganyifu.
Mshtakiwa huyo alijipatia fedha hizo kutoka kwa Ritha Remi baada ya kudanganya kuwa fedha hizo zitatumika kwa ajili ya biashara wakati akijua si kweli.
Katika shtaka lingine tarehe na mkoa huo kwa lengo la kudanganya mshtakiwa huyo alighushi namba ya utambulisho ya mlipa kodi (TIN), ya Septemba 19, mwaka 2016 kwa lengo la kuonesha kwamba ilitolewa na kamishna wa Kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wakati akijua si kweli.