Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kesi ya kina Mbowe yapigwa kalenda, sababu yatajwa

89236 Mboweeepic Kesi ya kina Mbowe yapigwa kalenda, sababu yatajwa

Fri, 20 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kesi ya jinai inayowakabili viongozi wa tisa wa Chadema akiwemo mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe imekwama kusikilizwa leo Alhamisi Desemba 19, 2019 na kuahirishwa Jumatatu ijayo.

Kesi hiyo ilipangwa kuendelea leo Alhamisi Desemba 19, 2019 katika hatua ya usikilizaji wa utetezi na upande wa mashtaka ulitarajiwa kumfanyia udodosaji mshtakiwa wa tisa, Ester Bulaya ambaye ni mbunge wa Bunda.

Wakili wa utetezi, John Mallya ameiomba mahakama hiyo kuahirisha usikilizaji huo kutokana na kiongozi wa jopo la mawakili wa utetezi, Peter Kibatala kutokuwepo.

Wakili Mallya amesema Kibatala ndiye aliyemwandaa shahidi huyo lakini leo ameshindwa kufika mahakamani kwa sababu amepata dharura ya kifamilia.

“Hatuko tayari kuendelea ingawa shahidi yupo kizimbani, lakini aliandaliwa na wakili Kibatala ambaye amepata dharura ya kifamilia, tunaomba ahirisho hadi tarehe nyingine,” amesema  Mallya.

Ombi la upande huo wa utetezi limepingwa na jopo la mawakili wa Serikali waliodai kuwa sababu zilizotolewa na upande huo hazina msingi, si za kisheria.

“Ni hatari kwa mahakama kuingia katika mtego huu wa kuahirisha cross examination (udodosaji) kwa sababu ya kutokuwepo wakili mmoja, katika kesi hii kuna jopo na mawakili wa utetezi,” amesema wakili wa Serikali mkuu Paul Kadushi aliyetaka kuahirishwa kwa muda mfupi, si mrefu.

Akitoa uamuzi Hakimu Mkazi Mkuu,  Thomas Simba amekubaliana na maombi hayo na kuamua kesi hiyo iendelee Jumatatu Desemba 23, 2019 ili mawakili hao wa utetezi wapate muda wa kupitia utetezi wa mshtakiwa.

Pia, Hakimu Simba amekubali kuahirisha kesi hiyo leo kwa kuwa hati ya kusafiria ya mshtakiwa huyo ambayo upande wa mashtaka uliiomba kuitumia wakati wa udodosaji wake, bado haijawasilishwa na akaamuru iwasilishwe leo.

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni katibu mkuu, Dk Vicent Mashinji; naibu katibu mkuu, John Mnyika (Bara) na Salum Mwalimu (Zanzibar); Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko; Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini); Halima Mdee (Kawe); John Heche (Tarime Vijijini);

Washitakiwa hao wanakabiliwa na makosa 13 likiwemo la kula njama  ambapo wote wanadaiwa kuwa  Februari Mosi na 16, 2018, Dar es Salaam waliku?a njama ya kutenda kosa la kufanya mkusanyiko usio halali na kukiuka tamko kutawanyika.

Chanzo: mwananchi.co.tz