Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kesi ya kina Mbowe yakwama tena

Kesimbowepic Kesi ya kina Mbowe yakwama tena

Thu, 10 Feb 2022 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Kesi ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu imeshindikana kuendelea leo baada ya upande wa Jamhuri kusema shahidi wao wa 13 bado amepumzishwa hospitalini.

Kesi hiyo ambayo ingeendelea leo Alhamisi Februari 10, 2022 kwa shahidi wa 13 wa upande wa mashtaka Mkaguzi wa Polisi, kutoka Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi, Mkoa wa Kipolisi Temeke, Tumaini Swila kuendelea kuhojiwa na upande wa utetezi.

Shahidi huyo jana wakati akiendelea kuhojiwa na Wakili wa upande wa utetezi Peter Kibatala, alisimama ghafla na kuieleza Mahakama kuwa hajisikii vizuri hali iliyosababisha Jaji Joachim Tiganga anayesikiliza kesi hiyo kuiahirisha hadi leo.

Leo, katika mahakama hiyo Wakili wa Serikali Mwandamizi, Nassoro Katuga aliiambia Mahakama kuwa shahidi wao amepumzishwa kutokana na ushauri wa daktari wake na kuiomba Mahakama iahirishe kesi mpaka Jumatatu.

Hata hivyo, upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili Peter Kibatala ulipinga ahirisho la mpaka Jumatatu wakitaka kesi hiyo kuendelea kesho Ijumaa.

Akitoa uamuzi, Jaji Tiganga amesema amekubaliana na ombi la upande wa utetezi la kuahirisha kesi hiyo mpaka Jumatatu Februari 14 kwa kuwa suala la afya ni nyeti huku akiuagiza upande wa mashtaka kuja na shahidi huyo na kama atakuwa bado mgonjwa wapeleke shahidi mwingine.

Advertisement Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine ni Halfan Bwire Hassan, Adamu Hassan Kasekwa maarufu kama Adamoo na Mohamed Abdillahi Ling’wenya.

Soma hapa kilichojiri mahakamani leo

Mawakili wa pande zote wameshaingia katika ukumbi wa mahakama pamoja na washtakiwa

Jaji Joachim Tiganga naye ameingia katika ukumbi wa mahakama

Mawakili wa pande zote wanajitambulisha

Jaji anawaita majina washtakiwa kuanzia mshtakiwa wa kwanza hadi wa nne

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Nassoro Katuga anasimama kwa ajili ya kutoa muhtasari

Katuga: Mheshimiwa Jaji shauri hili limekuja kwa ajili ya kuendelea na ushahidi, ambapo shahidi wa 13 Mkaguzi Tumaini Swila kuendelea kuhojiwa na upande wa utetezi.

Katuga: Lakini tangu jana shahidi wa 13 kwa hali yake aliyokuwa nayo, imepeleka jana hiyohiyo kupumzishwa kwa masaa kadhaa na dakatri wake ameomba aendelee kupumzishwa hapo hospitali.

Katuga: Daktari ameshauri shahidi wetu aendelee kupumzishwa na upande wa Jamhuri tunaona suala la ugonjwa lipo nje ya uwezo wa binadamu.

Kwa maana hiyo tunakubaliana na ushauri wa dakatri kuwa shahidi huyu aendelee kupumzika.

Kwa jana ilikuwa ni ngumu kutafuta shahidi mwingine ambaye pengine leo angetakiwa kuja na upande wa Jamhuri tunatambua uzito wa shauri hili.

Katuga: Kwa uzito huu tunaiomba mahakama ione hilo.

Katuga: Kwa hali hiyo tunaomba kesi hii iahirishwe hadi Jumatatu kwa ajili ya shahidi huyu kuendelea au kama atakuwa anaumwa basi tunaomba kuendelea na shahidi mwingine hiyo siku ya Jumatatu.

Tunaomba pia kuwasilisha nakala ya matibabu ya daktari ambayo imeletwa na ndugu wa shahidi lakini nakala ‘original’ italetwa na shahidi mwenyewe.

Kibatala: Mheshimiwa Jaji naomba dakika moja tuipitie nakala hii.

Karani anampatia Kibatala nakala ya taarifa ya shahidi kutoka hospitali anayopatiwa matibabu.

Kibatala: Nimesikia hoja ya rafiki yangu, ndugu yangu Katuga, nilianza na hii nyaraka hii iliyotoka hospitali.

Kibatala: Jana niliomba shahidi aniletee nyaraka ya karatasi kutoka hospitali ya Serikali na hiyo ni kwa mujibu wa sheria.

Kibatala: Hii nyaraka walioleta wenzetu inatoka hospitali ya TMJ na hii sio hospitali ya Serikali na nyaraka hii bado inazidi kuniweka katika wasiwasi kwangu na kwa upande wa utetezi.

Kibatala: Naomba mahakama ione sababu za kuahirishwa hazina maana.

Kibatala: Naomba tarehe ijayo waleta shahidi kwa sababu kesi hii ni nzito na kisheria kwa sababu imeletwa katika Mahakaka hii inatakiwa kuisha ndani ya miezi tisa.

Kibatala: Kuhusu kuahirisha hadi Jumatatu ...sisi tunaona Jumatatu ni mbali na saizi ni saa nne hivyo tunaona wenzake wana muda wa kutosha kutafuta shahidi, hivyo ni vizuri kesi hii tukaendelea nayo kesho ili tusiipoteze siku ya kesho.

Akijibu hoja hizo: Katuga amesema suala ya kuja na shahidi mwingine wamelichukua na watakufanyia kazi.

Katuga: Suala la kuleta cheti cha hospitali ya Serikali tunaomba kuikumbusha mahakama yako, shahidi huyu tangu anaanza ushahidi wake amekuwa anakuomba ruhusa mara kwa mara kwenda msalani na kwa maelezo yake alikuwa anatibiwa hapo na daktari wake ndo anajua ugonjwa wake.

Katuga: Mgonjwa kwenda kwa daktari wake anayemuamini ni nusu ya tiba.

Katuga: Kama wenzetu hawaamini wanaweza kwenda hapo kujiridhisha kwa daktari kwa mujibu wa maadili ya kazi yake. Kwa hiyo sisi hatuwezi kuidanganya mahakama.

Katuga: Kuhusu suala la kuahirisha mpaka Jumatatu, sisi tusingeweza kuisumbua mahakama kuwa tunaweza kuendelea kesho lakini tukaja na taarifa nyingine.

Katuga: Mashahidi wetu wengine ni wastasfu na wanatokea sehemu mbalimbali.

Katuga: Sasa hatupendi kuiahidi mahamama kwamba kesho tunaweza kuendea badala yake tukaja na the same stori. Tunaona kuwa ni busara kuahirisha mpaka Jumatatu.

Jaji Tiganga: Nimesikia hoja zilizotolewa na upande wa mashtaka kuhusu ombi la ahirisho.

Jaji: Kwa kuwa suala la afya ni nyeti na katika mahakama zetu suala la afya limekuwa ni sababu ya ahirisho.

Jaji: Mahakama ilisema shahidi alete uthibitisho wa taasisi alikotibiwa na si kwa details za ugonjwa wake na Mahakama haikuelekeza kuwa iwe ni hospitali ya Serikali maana kwenda huko ni kuingilia majukumu ambayo si yake kumpangia mtu akatibiwe wapi.

Jaji: Upande wa Jamhuri umesema unaogopa kuidanganya mahakama kuwa kesho wanaweza kuendelea lakini wakaja hapa na sababu nyingine na kwa sababu kesi hii inahusisha watu wengi na mawakili basi itakuwa ni kuharibu muda wao.

Jaji: Busara inaelekeza kuahirisha hadi Jumatatu tarehe ambayo upande wa mashtaka wamesema wanaweza kumpata shahidi huyo kuendelea na ushahidi wake au kuwa na shahidi mbadala.

Jaji: Hivyo ninaahirisha shauri hili mpaka Jumatatu na ninaelekeza upande wa mashtaka waje na shahidi huyu siku hiyo ili kama atakuwa vizuri aendelee na ushahidi wake na kama atakuwa hawezi basi waje na shahidi mbadala.

Jaji: Hivyo Naahirisha kesi hii hadi Jumatatu Februari 14, 2022 itakapokuja kwa ajili ya kuendelea.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz