Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kesi ya kina Malinzi kusikilizwa Desemba 5

28482 Malizni+pic TanzaniaWeb

Fri, 23 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kesi inayomkabili, aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi na wenzake wanne imesogezwa mbele hadi Desemba 5, mwaka huu.

Kesi hiyo inayosikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam itaendelea kusikiliza ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka.

Awali kesi hiyo ilipangwa kuendelea kusikilizwa jana kwa ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka, lakini ilishindikana kwa sababu mawakili wa serikali wanaoiendesha kesi hiyo Shadrack Kimaro na Leonard Swai walikuwa katika majukumu mengine. Baada ya Mahakama kufahamishwa hilo na kiongozi wa jopo la mawakili wa upande wa utetezi, Richard Rweyongeza kutokuwa na pingamizi Hakimu, aliamua kuiahirisha.

Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri alipanga kesi hiyo kuendelea kusikilizwa kwa ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka Desemba 5, 2018.

Kesi hiyo, ipo katika hatua ya kutolewa kwa ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka ambapo shahidi wa nane ambaye ni Katibu Mkuu wa TFF, Kidao Mzigama Wilfred, 41, amemaliza kutoa ushahidi wake hivyo ataendelea shahidi wa Tisa.

Washtakiwa katika kesi hiyo mbali na Malinzi, 57, wengine ni aliyekuwa Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa Joas Selestine, 46, na Mhasibu wa TFF, Nsiande Isawayo Mwanga (27).

Meneja wa Ofisi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Miriam Zayumba na Karani wa TFF, Flora Rauya ambao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 30 katika kesi ya jinai namba 213 ya mwaka 2017 yakiwamo ya kula njama, kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji wa fedha wa Dola 173,335 za Marekani na Sh 43.1 milioni.

Malinzi, Mwesigwa na Nsiande wapo rumande kwa kukabiliwa na mashtaka ya utakatishaji wa fedha kuwa miongoni mwa mashtaka ambayo kwa mujibu wa sheria hayana dhamana huku wenzao Zayumba na Frola wakiwa nje kwa dhamana.



Chanzo: mwananchi.co.tz