Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kesi ya dhahabu ya Sh27 bilioni yapigwa kalenda

38817 KESI+PIC Kesi ya dhahabu ya Sh27 bilioni yapigwa kalenda

Thu, 31 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwanza. Shauri namba 1/2019 la uhujumu uchumi, rushwa na kutakatisha fedha dhidi ya watu 12 wakiwemo askari polisi wanane katika mahakama ya hakimu mkazi Mwanza limetajwa leo Jumatatu Januari 28, 2019 na kuahirishwa hadi Februari 11, 2019 kwa kuwa upelelezi haujakamilika.

Wakili wa Serikali, Castus Ndamugoba ameiambia Mahakama kuwa upelelezi wa shauri hilo haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa.

Kwa mara ya kwanza, washtakiwa walifikishwa mahakamani Januari 11, 2019 wakidaiwa kuhusika na sakata la kilo 319.59 za dhahabu yenye thamani ya zaidi ya Sh27.018 bilioni na fedha taslim Sh305 milioni zilizokamatwa zikisafirishwa kutoka Mwanza kwenda Geita.

Mbele ya hakimu mkazi, Gwai Sumaye, mawakili watatu wa Serikali, Castus Ndamugoba, Robert Kidachi na Jackaline Nyantoro waliieleza mahakama kuwa washtakiwa walitenda makosa hayo kati ya Januari 4 na 5, 2019.

Wanaokabiliwa na shauri hilo ambao hawakutakiwa kujibu lolote kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na uwezo kisheria wa kusikiliza shauri hilo ni aliyekuwa mkuu wa operesheni mkoani Mwanza, mrakibu mwandamizi wa polisi, Morice Okinda, E. 6948 D/CPL. Kasala, F. 1331 PL. Matete, G. 6885 D/C Alex na G. 5080 D/C Maingu.

Wengine ni G. 7244 D/C Timothy, G. 1876 D/C Japhet, H. 4060 D/C David Kadama, Hassan Saddiq, Emmanuel Mtemi, Kisabo Nkinda ambaye pia anafahamika kwa jina la Paulo Nkinda na Sajid Hassan.

Kama ilivyokuwa Januari 11, 2019 washtakiwa walipofikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza, leo pia ulinzi uliimarishwa kuanzia kwenye msafara wa kutoka na kurejea mahabusu ya gereza la Butimba ambapo magari matano yaliyosheheni askari wenye silaha yalisindikiza msafara huo.

Tukio la kukamatwa kwa shehena ya dhahabu na mamilioni hayo ya fedha taslim lilitokea Januari 5, 2019 baada ya vyombo vya dola kupata taarifa kutoka kwa raia wema.



Chanzo: mwananchi.co.tz