Kesi ya Elpidius Edward (22) anayedaiwa kuvamia Kanisa kuu la Kiaskofu Jimbo la Geita na kufanya uharibifu wa mali za Sh48.2 milioni imeshindwa kuendelea baada ya Mahakama kuelezwa wakili anayesimamia kesi hiyo ni mgonjwa.
Kesi hiyo namba 62/2023 imekuja katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Geita kwa ajili ya upande wa mashtaka kuendelea kutoa ushahidi.Akitoa ombi la ahirisho mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Johari Kijuwile anayesikiliza kesi hiyo,Wakili wa Serikali, Scollastica Teffe ameieleza Mahakama licha ya kesi hiyo kuja kwa ajili ya kusikilizwa, wakili anayeisimamia ameshindwa kufika kwakuwa ni mgonjwa.
Kufuatia ombi hilo Hakimu Mkazi Mfawidhi, Kijuwile ameiahirisha hadi Julai 25, 2023 itakapokuja kwa ajili ya upande wa mashtaka kuita mashahidi wengine.
Tayari mashahidi wanne kati ya 20 wametoa ushahidi wao akiwemo daktari kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita, Christopher Matola aliyeileza Mahakama kuwa vipimo alivyomfanyia mshatakiwa vilionyesha hakuwa na tatizo la afya ya akili.
Mshatakiwa Elpidius ambaye ni Mkazi wa Mtaa wa Katundu mjini Geita anashtakiwa kwa makosa mawili likiwemo la kuingia katika jengo la Kanisa Katoliki Geita kinyume na kifungu cha 294 (1) na (2) cha kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022.Shtaka la pili anadaiwa kuharibu mali zenye thamani ya Sh 48.2 milioni kinyume na kifungu namba 226 (1) cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022.
Mshatakiwa amerejeshwa mahabusu kutokana na kushindwa kutimiza masharti ya dhamana yanayomtaka kuwa na wadhamini wawili watakaosaini hati ya fedha taslimu Sh24.1 milioni au mali isiyo hamishika yenye thamani hiyo.