Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kesi ya Zitto yakwama, shahidi yupo kwenye Oparesheni maalum

51315 Pic+zitto

Wed, 10 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar Es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imepanga siku mbili mfululizo, kusikiliza ushahidi wa upande wa mashtaka katika kesi ya uchochezi  inayomkabili, Mbunge wa Kigoma Mjini(Act- Wazalendo), Zitto Kabwe.

Kesi hiyo itaanza kusikilizwa kuanzia April 24 hadi 25, mwaka huu ambako Zitto anakabiliwa na mashtaka matatu ya uchochezi, katika mahakama hiyo.

Uamuzi huo umetolewa leo, April 9, 2019 na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Huruma Shaidi, baada ya upande wa mashtaka kuieleza mahakama kuwa shahidi aliyepaswa kutoa ushahidi yupo kwenye oparesheni maalumu ya Jeshi la Polisi.

"Kesi hii nitaisikiliza kwa siku mbili mfululizo kuanzia April 24 hadi 25, hivyo upande wa mashtaka mjipange kuleta mashahidi wa kutosha ili kesi hii iweze kumalizika muda uliopangwa," alisema Hakimu Shaidi.

Awali, wakili wa Serikali Mkuu, Tumaini Kwema akisaidiana na Faraji Nchimbi alidai kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kuanza kusikiliza ushahidi, lakini shahidi aliyepaswa kutoa ushahidi yupo kwenye oparesheni maalumu ya Jeshi la  Polisi.

"Kwa bahati mbaya shahidi ambaye tulimtegemea kuja kutoa ushahidi yupo katika operesheni maalum ya Jeshi la  Polisi" amedai Kweka.

"Kutokana na hali hiyo, tunaiomba mahakama itupe tarehe fupi ili tuweze kuendelea na usikilizwaji wa ushahidi," amedai Kweka.

Kweka baada ya kueleza hayo, wakili wa Zitto, Peter Kibatala akisaidiana na Steven Mwakibolwa, wamedai kuwa hawana pingamizi juu ya maelezo ya upande wa mashtaka.

Hakimu Shaidi baada ya kusikiliza hoja hizo, aliahirisha kesi hiyo hadi April 24 na 25, 2019 itakapoanza kusikilizwa na kuutaka upande wa mashtaka kuhakikisha kuwa wanaleta mashahidi wa kutosha.

Zitto alifikishwa Mahakama ya Kisutu kwa mara ya kwanza, Novemba 2, 2018 kujibu mashtaka matatu ya uchochezi katika kesi ya jinai namba 327/2018.

Katika kesi ya msingi, Zito anadaiwa kutenda makosa hayo, Oktoba 28,2018 katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ofisi za  makao makuu ya chama cha ACT Wazalendo.

Katika shtaka la kwanza, anadaiwa kuwa siku hiyo akiwa katika mkutano na waandishi wa habari kwa nia ya kuleta chuki miongoni mwa wananchi wa Tanzania dhidi ya Jeshi la polisi alitoa maneno ya uchochezi.

Alitoa maneno ya uchochezi kuwa "watu ambao walikuwa ni majeruhi katika tukio la mapambano baina ya wananchi na polisi, wakiwa wamekwenda hospitali kupata matibabu katika kituo cha afya cha Nguruka, polisi wakapata taarifa kuwa kuna watu wanne wamekwenda hospitali kituo cha afya Nguruka kupata matibabu wakawafuata kule wakawaua."

Inadaiwa kuwa maneno hayo yalikuwa ya uchochezi yenye kuleta hisia ya hofu na chuki.

Soma zaidi: Zitto mgonjwa, kesi yake yakwama, hakimu atoa neno

 



Chanzo: mwananchi.co.tz