Dar es Salaam. Kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili, Abdul Nsembo maarufu Abdulkandida (45) na mkewe, Shamim Mwasha(41) inasubiri majibu ya kielelezo kutoka kwa mkemia mkuu wa Serikali ya Tanzania.
Hayo yameelezwa na wakili wa Serikali, Simon Wankyo leo Jumatatu Julai 8, 2019 mbele ya hakimu mkazi mfawidhi, Kelvin Mhina kuwa kesi hiyo imekuja kwa ajili ya kutajwa kinachosubiriwa ni majibu ya kielelezo kutoka kwa mkemia huku akiomba tarehe nyingine ya kutajwa.
Juni 24, 2019 upande wa mashtaka pia ulisema kesi hiyo inasubiri ripoti ya mkemia huyo.
Wakili wa utetezi, Hajra Mungula amedai washtakiwa wako ndani na hawana dhamana na kuutaka upande wa mashtaka kufuatilia kielelezo hicho ili majibu yapatikane kwa wakati.
Hakimu Mhina baada ya kusikiliza maelezo ya hayo ameahirisha kesi hiyo hadi Julai 22, 2019 kwa ajili ya kutajwa na washitakiwa wamerudishwa rumande.
Shamimu ambaye ni mmiliki wa Blog 8020 Fashion na mumewe wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 36/2019.
Pia Soma
- Dk Kigwangalla ampoza Makamba mtandaoni
- TRA: Hatujapata tatizo stempu za kielektroniki
- VIDEO: Diamond awazawadia magari ya kifahari mama yake, Tanasha
- Lukuvi awasili kutatua mgogoro wa ardhi wa miaka 42
Wanadaiwa kusafirisha dawa za kulevya aina ya Heroin zenye uzito wa gram 232.70, wakati wakijua kufanya hivyo ni kosa kisheria.
Wanadaiwa kutenda kosa hilo, Mei mosi, 2019 katika eneo la Mbezi Beach, jijini Dar es Salaam.