Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kesi ya Sabaya yakwama tena

Sabaya Kesi Pic Kesi ya Sabaya yakwama tena

Thu, 4 Nov 2021 Chanzo: mwananchidigital

Kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake sita leo Alhamisi Novemba 4, 2021, imeahirishwa tena baada ya mtuhumiwa huyo wa kwanza kudaiwa kuendelea kuumwa.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha ilipanga shauri hilo namba 27, 2021 kuendelea kusikilizwa leo ambapo shahidi wa saba wa jamhuri ambaye ni Ofisa wa Tehama wa Benki ya CRDB Kanda ya Kaskazini, Jofrey Nnko angeendelea kutoa ushahidi wake.

SOMA: Sabaya mgonjwa, kesi yaahirishwa Akizungumza leo mahakamani hapo, Wakili Mosses Mahuna anayemtetea Sabaya aliieleza mahakama kuwa mtuhumiwa huyo wa kwanza bado ni mgonjwa na kuwa ametoa ruhusa kesi hiyo iendelee kusikilizwa bila yeye kuwepo.

Hii ni mara ya pili mtuhumiwa huyo kushindwa kufika mahakamani hapo ambapo jana Novemba 3 pia alishindwa kufika mahakamani akidaiwa kuumwa akiwa gerezani.

Wakili wa Jamhuri, Ofmed Mtenga aliiomba mahakama kuahirisha kesi hiyo hadi ruhusa ya maandishi ya mtuhumiwa ya shauri kuendelea bila yeye kuwepo iwasilishwe mahakamani hapo.

Hakimu Kisinda alikubaliana na maombi hayo na kuahirisha kesi hadi kesho itakapoendelea na usikilizwaji baada ya kibali cha maandishi cha mtuhumiwa huyo kuruhusu kesi hiyo iendelee bila yeye kuwepo kitakapowasilishwa mahakamani hapo.

Oktoba 27, 2021 Nnko alitoa ushahidi wake ambapo jamhuri waliomba mahakama iahirishe ushahidi wa shahidi huyo hadi pale shahidi wa nane atakapotoa ushahidi wake kwani ushahidi wa shahidi huyo wa nane atakaoutoa utahusisha nyaraka pamojaa ripoti ambazo zimezungumziwa na shahidi wa saba.

Chanzo: mwananchidigital