Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kesi ya Sabaya kuanza kusikilizwa leo

604a3caac74b662914174367cc7bec6c.jpeg Kesi ya Sabaya kuanza kusikilizwa leo

Fri, 2 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

KESI ya unyang’anyi wa kutumia silaha na kupora fedha shilingi 425,000 na vitu vya thamani inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya {34} na wenzake wawili inatarajiwa kuanza kusikilizwa leo katika Mahakama ya Wilaya ya Arusha.

Awali Sabaya na wenzake, Sylivester Nyengu (26) na Daniel Mbura {38} walisomewa maelezo ya awali na kusomewa mashitaka mawili ya unyang’anyi wa kutumia silaha na upepelezi wa kesi hiyo umekamilika.

Mashitaka hayo yalisomwa na mwendesha mashitaka wa serikali,Tarsila Gervas mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Arusha, Salome Mshasha.

Ilidaiwa mahakamani Februali 9 mwaka huu kuwa washitakiwa hao wakiwa na silaha katika mtaa wa Bondeni jijini Arusha walimpora Bakari Msangi shilingi 390,000 fedha taslimu.

Mahakama ilielezwa kuwa kabla ya kumpora walimpigia kwa ngumi, mateke ,makofi, kichwani na kumtisha kwa silaha kabla ya kutokomea na fedha hizo.

Gervas alisoma shitaka la pili la unyang’anyi wa kutumia silaha lililokuwa likiwakabili Sabaya, Nyengu na Mbura.

Ilidaiwa kuwa Februali 9 mwaka huu ndani ya Jiji la Arusha washitakiwa kwa pamoja wakiwa na silaha walimpora Ramadhani Rashid simu ya mkononi aina ya Tecno, fedha shilingi 35,000.

Mahakama ilielezwa kuwa kabla ya kufanya uhalifu huo Rashid alipigwa ngumi, mateke, kichwa na makofi.

Gervas aliwasomea watuhumiwa wote watatu maelezo ya awali na watuhumiwa wote walikana kutenda makosa hayo na kesi iliahirishwa hadi leo Julai 2 itakapoanza kusikilizwa.

Katika mashitaka mengine manne,Sabaya na wenzake watatu wanadaiwa kuongoza genge la uhalifu ,uhujumu uchumi, utakatishaji fedha haramu, matumizi mabaya ya madaraka na kuomba rushwa ya shilingi milioni 90.

Wengine walioshtakiwa na Sabaya ni pamoja na Enock Togolani Mnkeni {41} Mkazi wa Arusha, mshitakiwa wa tatu Watson Stanley Mwahomange {27} maarufu kwa jina la Malingumu , mshitakiwa wa nne ni John Odemba Aweyo.,

Upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kesi hiyo iliahirishwa hadi Julai 2 mwaka huu.

Kesi hiyo iliahirishwa jana na mwendesha mashitaka wa serikali ambaye pia ni Mkurugenzi Msaidizi wa ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa serikali{DPP},Tumaini Kweka mbele ya Hakimu Mfawidhi Mkoa wa Arusha, Martha Mahumbuga.

Awali mwendesha mashtaka,Tumaini Kweka mbele ya Hakimu Mfawidhi Mahumbuga aliwasomea shitaka la kwanza la uhujumu uchumi linalowakabili washitakiwa wote.

Ilidaiwa kuwa Sabaya akijua ni mtumishi wa umma yeye na wenzake Januari 20 mwaka huu ndani ya Jiji la Arusha alidaiwa kuongoza genge lake la uhalifu kutenda uhalifu.

Kweka alisoma shitaka la pili lililokuwa likimkabili Sabaya kuwa Januari 20 mwaka huu ndani ya Jiji la Arusha akiwa Mkuu wa Wilaya alishiriki kushawishi rushwa ya shilingi milioni 90 kutoka kwa mfanyabishara, Francis Mrosso mkazi wa kwa Mrombo ili aweze kumsadia katika kesi ya jinai ya ukwepaji kodi iliyokuwa ikimkabili.

Katika shitaka la tatu ilidaiwa kuwa Januari 20 mwaka huu Sabaya ndani ya Jiji la Arusha aliomba rushwa ya shilingi milioni 90 kutoka kwa mfanyabiashara wa jijini hapo mkazi wa Kwa Mrombo ili aweze kumsaidia katika kesi iliyokuwa ikimkabili ya ukwepaji kodi.

Kweka alisoma shitaka la nne la utakatishaji fedha haramu lililokuwa likiwakabili washtakiwa wote sita kuwa Januari 20 mwaka huu ndani ya Jiji la Arusha na Mkoa walichukua fedha shilingi milioni 90 za Mrosso.

Chanzo: www.habarileo.co.tz