Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha imeondoa pingamizi la upande wa Jamhuri lililowasilishwa mahakamani hapo kupinga upande wa utetezi kumhoji shahidi namba sita wa upande wa Jamhuri kuhusu maelezo aliyoyatoa polisi katika kesi ya jinai namba 105 ya unyang’anyi wa kutumia silaha inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya na wenzake wawili.
Akitoa uamuzi huo mdogo, Hakimu Mwandamizi anayeendesha shauri hilo, Odira Amworo amesema baada ya kufuatilia vifungu vya sheriana kurejea kesi nyingine zilizopita, amebaini kuwa hakuna mwongozo unaoweka wazi sheria kuzuia mahojiano kama hayo.
Hapo juzi, Agosti 2, 2021, mahakama hiyo ilitupilia mbali ombi la wakili wa utetezi, Sylvester Kahunduka la kuomba kumhoji shahidi wa sita katika kesi hiyo Bakari Msangi ambaye anaonekana kutokumbuka maelezo aliyoandika polisi.