Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kesi ya Padri Soka yaiva, mashahidi 10 kuitwa

Sokaapiic Mashahidi Kesi ya Padri Soka yaiva, mashahidi 10 kuitwa

Wed, 12 Oct 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati upande wa mashtaka katika kesi ya ubakaji wa mtoto wa miaka 12 inayomkabili Padri Sostenes Bahati (41) wa Kanisa Katoliji Jimbo la Moshi ukisema utaleta mashahidi 10, upande wa utetezi umeiarifu mahakama kuwa itaegemea ushahidi kuwa mshtakiwa hakuwepo eneo la tukio siku ya tukio hilo.

Kisheria, ushahidi huo unaofahamika kama Alibi, ni pale mshtakiwa anapojitetea kuwa alikuwa mahali pengine wakati wa tukio hilo, na hutakiwa kutolewa taarifa mapema, ili upande wa mashtaka ujiandae kwa ushahidi huo.

Jana, Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi chini ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Salome Mshasha anayesikiliza kesi hiyo ilielezwa namna kosa hilo la ubakaji lilivyotendeka Agosti 12,2022 katika Parokia Teule ya Mt Dionis Arobagita iliyopo Kawawa wilaya ya Moshi.

Upande wa mashtaka ukiongozwa na wakili mwandamizi wa Serikali kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashitaka (NPS), Kassim Nassir ulimsomea mshtakiwa maelezo ya awali ya kosa hilo, katika usikilizwaji ambao unavuta hisia za baadhi ya wazazi.

Akimsomea maelezo hayo, wakili Nassir alidai siku ya tukio akiwa ofisini kwake katika Parokia Teule ya Mt. Dionis Arobagita, Padri anatuhumiwa kumbaka mtoto huyo wa kike mwenye umri wa miaka 12.

Siku hiyo, ilielezwa kuwa watoto wanaosoma mafundisho ya Kipaimara walikuwa wamefika kwa ajili ya mafundisho kama ilivyokuwa ada ofisini na mtoto huyo alikwenda ofisini kwa padri huyo kwa ajili ya kupata huduma ya kutubu dhambi zake.

Ilidaiwa baada ya kufika ofisini kwa padri, mtoto huyo alipiga magoti na kutubu dhambi zake na baadaye padri ilidaiwa alimshika na kumnyanyua na kuanza kumtomasa sehemu mbalimbali mwilini na baadaye kumbaka.

Baada ya kufanyiwa kitendo hicho, mtoto huyo alirudi nyumbani kwa wazazi wake na katika mazungumzo kati ya mtoto na mama yake ndipo alimweleza kuwa padri huyo amekuwa akimfanyia vitendo vya kikubwa.

Hiyo iliwasukuma wazazi wa mtoto huyo kuchukua hatua ya kwenda kituo cha polisi kutoa taarifa na mshtakiwa alikamatwa na baadaye kushtakiwa kwa kosa hilo. Hata hivyo, mshtakiwa anayetetewa na wakili wa kujitegemea, Edwin Silayo alikanusha maelezo hayo na kukiri tu kwamba alifanyiwa gwaride la utambulisho akiwa polisi na pia akakubali majina yake na anuani.

Wakili Nasiri alisema katika kesi hiyo wapo mashahidi 10 wa upande wa mashtaka na siku itakaposikilizwa mashahidi wanne watatoa ushahidi wao.

Hata hivyo, wakili Silayo aliomba kesi hiyo isianze kusikilizwa jana kwa maelezo ndio mara ya kwanza kukutana na mteja wake, hajapewa maelezo ya mlalamikaji kama sheria inavyotaka na pia hajapatiwa hati ya mashtaka.

Pia alisema mteja wake anakusudia kutumia ushahidi wa Alibi katika utetezi wake, hivyo aliomba apewe muda, ili awasilishe ilani ya kisheria, ombi lililoridhiwa na hakimu na kesi imepangwa kusikilizwa Oktoba 12.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live