Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kesi ya 'Mpemba wa Magufuli ' kuanza kuunguruma kesho Kisutu

58911 Mpembapic

Wed, 22 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kesho Jumatano Mei22, 2019 itaanza kusikiliza ushahidi wa upande wa mashtaka katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili, Yusuf Ali Yusuf maarufu ‘Mpemba wa Magufuli’.

Yusuf na wenzake watano, wanakabiliwa na mashtaka manne ya kujihusisha na biashara haramu ya meno ya tembo yenye thamani ya Sh785.6milioni.

Kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 53/2016 imepangwa kusikilizwa ushahidi kwa siku mbili mfululizo kuanzia Mei 22 hadi 23, 2019  katika mahakama hiyo.

Uamuzi huo umetolewa leo Jumanne Mei 21, 2019 na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba baada ya upelelezi wa kesi hiyo kukamilika na mkurugenzi wa mashtaka nchini (DPP), kuipa Mamlaka Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kusikiliza kesi hiyo.

"Kwa kuwa kesi hii ni ya muda mrefu tumeipanga siku mbili mfululizo kuisikiliza, yaani kesho( Mei 22 na 23, 2019) hivyo upande wa mashtaka mlete mashahidi wenu wa kutosha ili kesi hii iweze kusonga mbele,” amesema Hakimu Simba.

Awali, wakili wa Serikali Candid Nasua alidai kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kutajwa na kupangiwa tarehe ya kuanza kusikiliza ushahidi wa upande wa mashtaka.

Pia Soma

"Washtakiwa wote wapo mbele ya Mahakama yako na shauri hii limekuja kwa ajili ya kutajwa na kupangiwa tarehe ya kuanza kusikilizwa," alidai Nasua.

Nasua alidai  upande wa mashtaka unatarajia kuwa na mashahidi zaidi ya 10 na vielelezo vyenye idadi sawa na mashahidi, ambao watatoa ushahidi wao dhidi ya washtakiwa hao.

Baada ya Nasua kueleza hayo, wakili wa utetezi, Nehemia Nkoko akisaidiana na Hassan Kiangio, walidai kuwa hawana pingamizi juu ya tarehe hiyo.

Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi Mei 22 na 23, 2019 itakapoanza kusikilizwa ushahidi na washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na mashtaka yanayowakabili kutokuwa na dhamana.

Mbali na Yusuph(35), washtakiwa wengine katika kesi hiyo  ni Charles Mrutu(37), maarufu kama mangi mapikipiki na mkazi wa Mlimba, Morogoro; Benedict Kungwa(40), mkazi wa Mbagala Chamazi;  Jumanne Chima(30), maarufu kama JK na mkazi wa Mbezi;  Ahmed Nyagongo(33), dereva na mkazi wa Vikindu-Mkuranga na Pius Kulagwa(46)mfanyabiashara na mkazi wa Temeke.

Washtakiwa kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka manne, likiwemo la kujihusisha na mtandao wa ujangili.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa  wanadaiwa kati ya Januari, 2014 na Oktoba, 2016, katika maeneo ya Dar es Salaam, Tanga, Iringa na Mtwara, walijihusisha na mtandao wa ujangili kwa kukusanya na kuuza nyara za Serikali ambazo ni vipande 50 vya meno ya tembo vyenye thamani ya dola za Marekani 180,000 sawa na Sh 392,817,600 bila kuwa na kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori.

Katika shtaka la pili, Oktoba 26, 2016 wakiwa Mbagala Zakhem, walikutwa na vipande 10 vya meno ya tembo vyenye uzito wa kilo 13.85 vikiwa na thamani ya dola za Marekani 30,000 sawa na Sh 65, 469,600.

Shtaka la tatu, washtakiwa hao wanadaiwa, Oktoba 27, 2016, eneo la Tabata Kisukuru, walikutwa na vipande vinne vya meno vyenye uzito wa kilo 11.1 vikiwa na thamani ya dola za Marekani 15,000, sawa na Sh 32, 734,800.

Washtakiwa pia, wanadaiwa, Oktoba 29, 2016 walikutwa na vipande 36 vyenye  uzito wa kilo 58.55, vikiwa na thamani ya dola za kimarekani 135,000, sawa na Sh 294,613,200, bila kuwa na kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz