Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kesi ya Mkurugenzi Jamii Forum yaahirishwa tena

11616 Jamii+pic TanzaniaWeb

Tue, 17 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kesi ya kuzuia jeshi la polisi kufanya uchunguzi, inayomkabili, Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jamii Forum, Maxence Melo na mwenzake Micke William, imeshindwa kuendelea na ushahidi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Hii ni mara  ya tatu mfululizo kwa kesi hiyo kushindwa kuendelea na usikilizwaji wa ushahidi katika Mahakama hiyo, katika kipindi cha mwezi mmoja.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Patrick Mwita amedai leo Julai 17, 2018 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Thomas Simba, Wakili anayeendesha shauri hilo amepata udhuru.

"Kesi hii imekuja kwa ajili ya kuendelea na ushahidi, lakini Wakili anayeendesha shauri hili, Mutalemwa Kishenyi amepata udhuru asubuhi hii(Jana), hivyo anaomba kesi hii ipangiwe tarehe yoyote kuanzia kesho" amedai Mwita.

Hakimu Simba baada ya kusikiliza maelezo hayo, aliutaka upande wa mashtaka kuhakikisha wanaleta mashahidi wa kutosha ili kesi hiyo iweze kuisha kwa sababu ni kesi ya muda mrefu.

"Mlete mashahidi wa kutosha, kesi hii ni ya muda mrefu, tumeshakaa nayo hapa mahakamani vya kutosha " amesema Hakimu Simba.

Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 26 na Agosti mosi mwaka huu itakapoendelea na ushahidi.

Tayari mashahidi wanne wa upande wa mashtaka wameshatoa ushahidi wao dhidi ya washtakiwa hao.

Chanzo: mwananchi.co.tz