Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kesi ya Maimu, wenzake yapigwa kalenda

Wed, 15 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili mkurugenzi mkuu wa zamani wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), Dickson Maimu na wenzake imeshindwa kuendelea kutokana na hakimu anayeendesha shauri hilo kupata udhuru.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni meneja biashara wa Nida, Aveln Momburi, mkurugenzi wa kampuni ya Aste Insurance Brokers, Astery Ndege, ofisa usafirishaji, George Ntalima na mkurugenzi wa sheria, Sabina Raymond.

Wakili wa Serikali, Janeth Magoho aliieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Jumanne Mei 14, 2019 kuwa shauri hilo lilikuja kwa ajili ya kutajwa na hakimu anayeendesha shauri hilo amepata udhuru.

Magoho alidai kuwa upelelezi bado haujakamilika na aliiomba mahakama hiyo ipange tarehe nyingine.

Baada ya maelezo hayo Hakimu Mkazi, Augustina Mbando aliahirisha shauri hilo hadi Mei 28, 2019 litakapokuja kwa ajili ya kutajwa.

Katika kesi ya washtakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka 22 ya kughushi, mashtaka 43 ya kutumia nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri, mashtaka mawili ya kula njama, mashtaka 25 ya kutakatisha fedha na mashtaka matano ya kuisababishia hasara Nida.

Pia Soma

Pia washitakiwa wanakabiliwa na mashtaka mawili ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na moja la matumizi mabaya ya madaraka ambalo linamkabili Maimu na Sabina.

Katika mashtaka ya kwanza ya kula njama, Maimu, Ndege na Ntalima wanadaiwa, kati ya Julai 19, 2011 na Agosti 31,2015 wakiwa maeneo tofauti tofauti ndani ya jiji la Dar es Salaam walikula njama ya kufanya udanganyifu wa Sh1.175 bilioni dhidi ya Nida.

Pia Maimu anadaiwa kutakatisha fedha kiasi cha Sh1.175 bilioni kati Julai 19, 2011 na Agosti 31, 2015 ambapo anadaiwa kujihusisha moja kwa moja kuhamisha fedha hizo huku akijua ni zao la kosa la kughushi.

Chanzo: mwananchi.co.tz