Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kesi ya Lucky Vincent yakwama, kuendelea Novemba Mosi

20492 Pic+luck TanzaniaWeb

Wed, 3 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha. Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa Arusha, inatarajiwa kuendelea kusikiliza kesi ya ajali ya iliyouwa wanafunzi 32, walimu wawili na dereva wa gari la shule ya Lucky Vincent inayomkabili mmiliki wa shule hiyo, Innocent Moshi na Mwalimu Mkuu Msaidizi wa shule hiyo, Longino Nkana Novemba 1, 2018.

Katika kesi hiyo, Mmiliki wa shule hiyo, Moshi na mwalimu mkuu msaidizi, Nkana wanakabiliwa na makosa matano tofauti, kutokana na ajali hiyo, ambayo ilitokea katika mteremko wa mlima wa Rhotia, wilayani Karatu Mei 6, 2017.

Mmiliki wa shule hiyo ana mashtaka manne, kufanya biashara ya usafirishaji abiria bila kuwa na leseni, kuruhusu gari kutumika bila kuwa na bima pamoja na kushindwa kuingia mkataba na dereva mwajiriwa wake na kuzidisha abiria 13 katika basi lililopata ajali.

Makamu mkuu wa shule hiyo, Nkana anakabiliwa na shitaka moja la kuzidisha abiria 13 katika gari lililobeba wanafunzi ambalo lilipata ajali.

Kesi hiyo ambayo leo Oktoba 2, 2018, ilitarajiwa kuendelea kusikilizwa, lakini iliahirishwa kutokana na Hakimu Mfawidhi Niku Mwakayobe anayesikiliza kesi hiyo kuwa nje ya Mahakama kwa majukumu ya kikazi.

Katika kesi hiyo tayari, Jamhuri imekwishaita mashahidi sita na ilitarajiwa kuendelea na ushahidi.

Kutokana na kutokuwapo hakimu huyo, kesi hiyo ilitajwa mbele ya Hakimu Obadia Bwegego ambapo Wakili wa Serikali Khalili Nuda alimwomba hakimu huyo kuahirisha kesi hiyo kutokana na hakimu kuwa na dharura ya kikazi.

Hakimu Bwegego alikubaliana na maombi hayo na  kuahirisha kesi hiyo hadi, Novemba Mosi mwaka huu itakaposikilizwa na kuamuru dhamana za washitakiwa kuendelea.

Chanzo: mwananchi.co.tz