Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kesi ya Jamii Forum kusikilizwa siku tatu mfululizo

15602 Kesi+pic TanzaniaWeb

Wed, 5 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imepanga kusikiliza kwa siku tatu mfululizo, kesi ya kuendesha mtandao ambao haujasajiliwa nchini kwa kikoa cha .co.tz (Tanzania domain) inayomkabili, Mkurugenzi Mtendaji wa Jamii Media, Maxence Melo na mwenzake Micke William.

Uamuzi huo umetolewa leo Septemba 4, 2018 na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Huruma Shaidi, wakati shauri hilo lilipokuja kwa ajili ya kuendelea na ushahidi.

“Kesi hii tutaisikiliza siku tatu mfululizo kuanzia Septemba 24 hadi 26, hivyo upande wa mashtaka mje na mashahidi wa kutosha ili kesi hii iweze kuisha kwa sababu ni ya muda mrefu," amesema Hakimu Shaidi.

Kesi hiyo ya Jinai namba 458 ya mwaka 2016, ilipaswa leo, Septemba 4, 2018 kuendelea na ushahidi, lakini upande wa mashtaka hawakuwa na shahidi.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi alidai kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kuendelea na ushahidi lakini shahidi aliyepaswa kutoa ushahidi hakuwepo mahakamani, hivyo akaomba tarehe nyingine kwa ajili kuendelea na ushahidi.

Kutokana na maelezo hayo, Hakimu  Shaidi aliahirisha kesi hiyo hadi Septemba 24 ambako itasikilizwa hadi Septemba 26.

Tayari mashahidi watatu wa upande wa mashtaka akiwemo Peter Kayombi kutoka Ofisi ya Upelelezi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, wameshatoa ushahidi wao.

Katika ushahidi aliotoa Kayombi, alieleza Desemba 14, 2016 akiwa ofisini, aliitwa na Mkuu wa Upelelezi kanda maalum ya Dar es Salaam ZCO, Wambura na kukabidhiwa jalada lililokuwa linahusu watuhumiwa wanaomiliki tovuti ambayo haijasajiliwa kwa kikoa cha .co.tz.

"Baada ya kupokea jalada na kulisoma niligundua washtakiwa katika kesi hii ni Melo na Micke na wakati huo Melo alikuwa tayari amekamatwa, hivyo nilianza kumhoji kwa ajili ya kunipa maelezo kuhusiana na tovuti wanayoimiliki" alidai Kayombi.

Kayombi alidai Melo alimueleza ni kweli anaendesha tovuti ya Jamii Forum na aliisajili mwaka 2008 nchini Marekani.

"Baada ya kumhoji Melo, tulifanya utaratibu wa kumtafuta Micke na kwamba Januari 16, 2017 alipatikana na tukamhoji " alidai Kayombi.

Alidai baada ya kumhoji Melo, aliandika barua kwenda Tanzania Network Information Center (tzNIC), ili apate taarifa za Mtandao wa Jamii Forum kama imesajiliwa kwa kikao cha .co.tz.

Alidai, majibu yaliyotolewa na Tanzania Network Information Center, yalieleza Jamii Forum walisajiliwa kwa mara ya kwanza mwaka 2010 kama kikoa(.co.tz) na mwaka 2013 iliondolewa na mwaka 2016 ilisajiliwa tena kama Jamii Forum.co.tz lakini haikuwa ikitumia kikoa hicho.

Katika Kesi ya msingi, washtakiwa wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Desemba 9, 2011 na Desemba 13, 2016 katika eneo la Mikocheni wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Washtakiwa wanadaiwa kuendesha mtandao ambao haujasajiliwa nchini, yaani .tz (Tanzania domain) na kushindwa 'kutoa ushirikiano' kwa Jeshi la Polisi kwa kuzuia taarifa binafsi za wateja wa mtandao wake.

Chanzo: mwananchi.co.tz