Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kesi ya Gugai wa Takukuru kusikilizwa siku tatu mfululizo

82501 Gugai+pic Kesi ya Gugai wa Takukuru kusikilizwa siku tatu mfululizo

Fri, 1 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu itasikiliza kwa siku tatu mfululizo ushahidi wa kesi inayomkabili aliyekuwa mhasibu mkuu wa Takukuru, Godfrey Gugai.

Gugai na wenzake wawili wanakabiliwa na mashtaka 39

yakiwemo ya kutakatisha fedha na kughushi.

Leo Alhamisi Oktoba 31, 2019 Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Thomas Simba amepanga kesi hiyo kuendelea na ushahidi Novemba 11 hadi 13, 2019.

Hakimu Simba amepanga tarehe hizo baada ya shahidi wa 27 wa upande wa mashtaka, Mndima Msangi kutoa ushahidi wake dhidi ya Gugai.

Katika ushahidi huo, Msangi ambaye ni mwajiriwa wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kituo cha Tegeta, amedai  kuwa ndio aliyekwenda kwa Gugai kumfungia mashine ya Luku  katika nyumba ya ghorofa moja iliyopo Bunju wilaya ya Kinondoni. Akiongozwa na wakili wa Takukuru, Ipyana Mwakatobe, shahidi huyo amedai kabla ya kwenda kufunga mashine hiyo, alipewa fomu na kiongozi wake kuwa anatakiwa kwenda kufunga katika nyumba ya Gugai.

“Ile fomu niliyopewa ilikuwa na jina la mteja, namba ya simu na mchoro wa nyumba hivyo mimi nilitumia mchoro kufika katika nyumba ya Gugai na kumfungia mashine ya Luku” amedai Msangi ambaye aliajiriwa na shirika hilo, mwaka 1991.    

Msangi amedai baada ya kumaliza kufunga mashine ya mita, alisaini fomu maalumu kuonyesha kuwa amekamilisha zoezi la kumfunga Luku.

Baada ya kumaliza kutoa ushahidi, hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 11 hadi 13, 2019 na mshtakiwa huyo kurudishwa rumande.

Tayari mashahidi 27 wa upande wa mashtaka wameshatoa ushahidi katika kesi hiyo

Mbali na Gugai, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni George Makaranga na Leonard Aloys.

Kati ya mashtaka hayo 39, mashtaka 20 ni ya kutakatisha fedha na 19 ni ya kughushi.

Pia, Gugai anakabiliwa na kosa moja la kumiliki mali kinyume na kipato chake ambapo anadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Januari 2005 na Desemba, 2015.

Chanzo: mwananchi.co.tz