Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kesi ya Gugai kusikilizwa siku mbili mfululizo

51132 Pic+gugai

Mon, 8 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu inatarajia kusikiliza mashahidi sita watakaotoa ushahidi kwa siku mbili mfululizo katika kesi ya utakatishaji fedha na kumiliki mali zilizozidi kipato inayomkabili aliyekuwa Mhasibu Mkuu wa Takukuru, Godfrey Gugai na wenzake watatu.

Mbali na Gugai, washtakiwa wengine katika kesi hiyo, ni George Makaranga, Leonard Aloys na Yasin Katera.

Wakili wa Serikali, Awamu Mbagwa akiieleza mahakama hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba amedai kuwa shauri hilo lilikuja kwa ajili ya kusikilizwa.

Mbagwa ameomba shauri hilo liahirishwe na lipangiwe tarehe mbili mfululizo kwa ajili ya kusikilizwa na wanatarajia kuwa na mashahidi sita.

"Niliahidi kulifanyia kazi kuhusiana ushahidi hivyo tuliwasiliana na mahakama wamesema wameanza mchakato na wameahidi tupange siku mbili mfululizo na tumepanga mashahidi sita ambao watatoa ushahidi," amedai Mbagwa.

Mashahidi sita wanatarajiwa kutoa ushahidi mfululizo mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu katika kesi ya utakatishaji fedha na kumiliki mali zinazozidi kipato, inayomkabili Gugai.

Baada ya maelezo hayo, Hakimu Simba amesema siku litakayopangwa kusikiliza shauri hilo atahakikisha mashahidi wote wanasikilizwa hadi waishe hata kama itafika saa 12 jioni.

Simba ameahirisha kesi hiyo hadi Aprili18, mwaka huu itakapotajwa na kuanza kusikilizwa ushahidi Aprili24 na 25, 2019

Katika kesi ya msingi Gugai na wenzake wanakabiliwa na makosa 43. Kati ya hayo, makosa 19 ni ya kughushi, 23 ni utakatishaji fedha na moja ni kumiliki mali zinazozidi kipato halali ambalo linamkabili Gugai.

Gugai anakabiliwa na kosa la kumiliki mali kinyume na kipato chake, ambalo anadaiwa kulitenda kati ya Januari 2005 na Desemba 2015.

Inadaiwa kuwa akiwa Takukuru Dar es Salaam, alikuwa akimiliki mali za zaidi ya Sh3.6 bilioni ambazo hazilingani na kipato chake huku akishindwa kuzitolea maelezo.



Chanzo: mwananchi.co.tz