Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kesi ya Dk Pima na wenzake yakwama kusikilizwa

Pindi Picggggg Kesi ya Dk Pima na wenzake yakwama kusikilizwa

Thu, 20 Oct 2022 Chanzo: mwanachidigital

Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha imekwama kusikiliza kesi za uhujumu uchumi zinazomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, Dk John Pima na wenzake wanne baada ya mashahidi wa Jamhuri kutokuwepo mahakamani hapo.

Mbali na Dk Pima watuhumiwa wengine ni aliyekuwa Mkuu wa Idara ya Fedha katika halmashauri hiyo Mariam Mshana, aliyekuwa Mkuu wa Idara ya Mipango na Uchumi, Innocent Maduhu, Alex Daniel na Nuru Ginana (aliyekuwa mchumi).

Leo Alhamisi Oktoba 20, 2022 Mahakama hiyo ilipanga kuanza kusikiliza kesi mbili za uhujumu uchumi kati ya tatu kwa upande wa mashahidi wa jamhuri kuanza kutoa ushahidi wao.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Fadhil Mbelwa, Jamhuri iliwakilishwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Janeth Sekule huku utetezi ukiwakilishwa na Mawakili Edmund Ngemela, Sabato Ngogo na Jacob Msigwa.

Katika kesi ya uhujumu uchumi namba 3/2022, Wakili Janeth aliileza mahakama kuwa wanaomba tarehe nyingine ya kusikiliza kesi hiyo kufuatia mashahidi kutokuwepo mahakamani hapo huku wakisubiria hakimu wa kusikiliza kesi hiyo kama ilivyo elezwa katika hatua za awali.

Kufuatia hoja hiyo Hakimu Mbelwa alieleza kuwa kesi zote tatu zinazowakabili watuhumiwa hao ziko kwake na kama kuna zoezi la kutafuta hakimu mwingine au la ni la kiutawala.

“Hizi kesi zote tatu zilikuwa kwangu na kama kuna zoezi la kutafuta hakimu mwingine au la ni la kiutawala lakini haina maana kuna mtu ana hizi kesi zaidi ya mimi kwa sasa,na kwa kuwa hakuna shahidi tunaahirisha,” alieleza Hakimu huyo

Katika kesi ya uhujumu uchumi namba 4/2022 inayomkabili Dk Pima, Mariam, Maduhu na Daniel, Wakili Janeth aliieleza mahakama kuwa kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kuanza kusikilizwa pia ila mashahidi hawajaweza kufika.

Kesi zote mbili zimeahirishwa na zinatarajiwa kuanza kusikilizwa mfululizo kuanzia Novemba 8 hadi 10,mwaka huu, ambapo katika kesi namba 4/2022 jamhuri ilieleza mahakama kuwa inatarajia kuwa na mashahidi 14 na vielelezo 17.

Chanzo: mwanachidigital