Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kesi ya Bilionea Msuya: Washtakiwa wana kesi ya kujibu

Msuya Bilionea.jpeg Kesi ya Bilionea Msuya: Washtakiwa wana kesi ya kujibu

Mon, 18 Sep 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imewataka washtakiwa katika kesi ya mauaji ya Aneth Msuya, kujitetea dhidi ya kosa hilo linalowakabili, baada ya kuwaona wana kesi ya kujibu.

Mahakama ilitoa uamuzi huo juzi jioni baada ya upande wa mashtaka kufunga ushahidi.

Washtakiwa katika kesi hiyo namba 103 ya mwaka 2018 ni Miriam Mrita , mjane wa aliyekuwa mfanyabiashara maarufu wa madini mkoani Arusha, marehemu Erasto Msuya, maarufu Bilionea Msuya; na Revocatus Muyella.

Miriam na Muyella (maarufu Ray au Revoo) wanakabiliwa na kosa la mauaji ya Aneth, mdogo wa Bilionea Msuya, aliyeuawa kwa kupigwa risasi eneo la Mijohoroni wilayani Hai mkoani Kilimanjaro Agosti 7, 2013.

Aneth aliuawa Mei 26, 2016 kwa kuchinjwa nyumbani kwake Kibada, Kigamboni, wilayani Temeke (wakati huo), jijini Dar es Salaam.

Upande wa mashitaka ulifunga ushahidi juzi baada ya kuwaita mashahidi 25 kati ya 45 waliokuwa wametajwa awali na kuwasilisha vielelezo 17.

“Mheshimiwa Jaji shahidi huyu wa 25 ndiye wa mwisho. Hatukusudii kuita mwingine. Kwa hiyo tunafunga ushahidi na tunaiachia Mahakama ione kama wana kesi ya kujibu,” alisema kiongozi wa jopo la waendesha mashitaka, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Paul Kimweri.

Jaji Edwin Kakolaki aliwapa nafasi mawakili wa utetezi, Peter Kibatala na Nehemia Nkoko, ambao kwa nyakati tofauti walisema hawana pingamizi na kwamba, wanaiachia Mahakama ione kama washitakiwa wana kesi ya kujibu au la. “Mahakama baada ya kupitia ushahidi na vielelezo vya upande wa mashitaka imejiridhisha kuwa kuna kesi ya msingi ambayo imejengwa inayojitosheleza kuwafanya wajitetee, hivyo inatamka kwamba washtakiwa wana kesi ya kujibu,” alisema Jaji Kakolaki katika uamuzi wake.

Aliwafahamisha washtakiwa kuwa wana haki ya kutoa ushahidi wenyewe lakini pia wanaruhusiwa kuita mashahidi na wataweza kuulizwa maswali.

“Pia mna haki ya kukaa kimya, lakini ukitumia haki hiyo, Mahakama ina mamlaka ya kuchukulia vinginevyo kukaa kwako kimya jinsi ambavyo itaona inafaa na kuendelea kufanya maamuzi. Na katika kujitetea kwenu mnaweza kujitetea kwa kiapo,” alisema Jaji Kakolaki.

Alitoa nafasi kwa kila mshitakiwa kueleza ni haki gani atakayotumia. Wote walisema watajieleza kwa kiapo, wataita mashahidi na kuwasilisha vielelezo. Hata hivyo, hawakutaja idadi ya mashahidi.

Jaji Kakolaki alisema kwa kuwa muda wa kesi hiyo uliokuwa umepangwa kusikilizwa mfululizo mwezi mzima umeisha, aliiahirisha mpaka kikao kijacho kwa tarehe itakayopangwa na kwamba pande zote zitajulishwa.

Awali, shahidi wa 25 na wa mwisho wa upande wa mashitaka alifunga ushahidi baada ya kuhojiwa na mawakili wa utetezi kuhusu ushahidi wake wa msingi wakati akiongozwa na mwendesha mashtaka, wakili Kimweri.

Shahidi huyo, Getruda Mfuru (38), aliyekuwa mfanyakazi wa ndani wa marehemu Aneth, alisimulia mfululizo wa matukio ya kabla na baada ya mauaji ya mwajiri wake huyo wa zamani.

Sehemu ya maswali ya dodoso ambayo mawakili wa utetezi walimhoji shahidi huyo na majibu yake ni kama ifuatavyo:

Wakili Kibatala: Shahidi nyumba ya marehemu Aneth ilikuwa na vyumba vingapi?

Shahidi: Sifahamu.

Kibatala: Ulifika lini kwa Aneth kama kweli wewe ni Getruda?

Shahidi: Tarehe 4/1/2016.

Kibatala: Wewe ulikuwa unalala chumba kipi?

Shahidi: Kwa kweli sikumbuki.

Kibatala: Ndiyo maana tuna taarifa kwamba wewe si Getruda Peniel Mfuru halisi, miezi minne hujui nyumba ya Aneth ilikuwa na vyumba vingapi wala hukumbuki chumba ulichokuwa ukilala.

Kibatala: Baba yako ni nani vile?

Shahidi: Peniel Mfuru.

Kibatala: Birthday (siku ya kuzaliwa) yake ni lini?

Shahidi: Sikumbuki

Kibatala: Ndiyo maana nakwambai tuna taarifa kwamba wewe si Getruda bali ni Polisi na kituo chako ni Zanzibar.

Shahidi: Mimi si ofisa wa Polisi

Kibatala: Kama kweli wewe ni Getruda Peniel Mfuru uliwahi kukamatwa tarehe 27/5/2016?

Shahidi: Sikuwahi kukamatwa tarehe 27/5/2016.

Kibatala: Uliwahi kuwa na ugomvi na Polisi yeyote Kigamboni, kwa nini uanze kutunga haya?

Shahidi: Sijawahi kuwa na ugomvi na Polisi yeyote kutoka Kigamboni.

Kibatala: Simu uliyopewa na huyu mama (mshtakiwa wa kwanza, Miriam) ndiyo uliyokwenda nayo kwa Sabri (mpenzi wake wa Chanika) na Masama (kijijini kwao huko Kilimanjaro).

Shahidi: Ni tofauti

Kibatala: Laini ni nyingine au ile ile?

Shahidi: Simcard ilikuwa ileile

Kibatala: Sasa shahidi umekwenda kwa Sabri baada ya kutaarifiwa kifo cha Aneth na ulisema kuna watu walikwambia wanataka kwenda kufanya kazi kwa dada yako na ukasikia amechinjwa kinyama ni kweli Sabri alikushauri kwenda Polisi?

Shahidi: Ni kweli lakini kwa sababu ya woga sikwenda.

Kibatala: Mama wa watoto watatu dada yako amechinjwa na kuna watu walikutishia na sasa hawapo lakini hukwenda kuripoti?

Kibatala: Ulipofika kwenu Masama ulimweleza nani?

Shahidi: Mama yangu.

Kibatala: Anaitwa nani?

Shahidi: Elinisaria Ndosi

Kibatala: Lini ilikuwa?

Shahidi: Tarehe 28/5/2016 baada ya kufika nyumbani.

Kibatala: Alichukua hatua gani?

Shahidi: Alikuwa mgonjwa.

Kbatala: Mchungaji wako ni nani?

Shahidi: Kimaro

Kibatala: Ulimwambia mambo mazito kama haya?

Shahidi: Kwa kweli sikumwambia wala sikuwa na wazo hilo.

Kibatala: Kabla ya kupigiwa simu na Bibi Msuya, kuna mtu alikupigia kuwa bosi wako amechinjwa wewe uko wapi uje tukuhoji?

Shahidi: Hakuna aliyenipigia

Kibatala: Baada ya kutupa ile simu ulikuwa na namna nyingine ya kuwasiliana na (mshtakiwa Miriam) yule mama?

Shahidi: Sikuwa na namna nyingine.

Kibatala: Lakini ni mama huyo aliyekwambia atakupatia Sh50 bilioni. Ulikuwa na namna nyingine ya kumpata?

Shahidi: Sikuwa na namna nyingine na ndiyo maana niko hapa.

Kibatala: Unaweza kumwambia Jaji hizo Sh50 bilioni ungezipataje

Shahidi: Mimi sikuwa nazingatia kwenye Sh50 bilioni ila katika ushahidi wangu kujua nini kitakachoendelea.

Kibatala: Baada ya haya yote una damu yako (ndugu wa damu) Gongo la Mboto hukumwambia badala yake ukamwambia Sabri ambaye ni rafiki yako tu?

Shahidi: Nilimuita Sabri sababu ni rafiki yangu.

Wakili Nkoko: Shahidi, nitakuwa sahihi wewe ndiyo ulikuwa mtu pekee Aneth alikuwa akimwamini kubaki na mali zake zote kuanzia asubuhi mpaka jioni ikiwemo nyumba?

Shahidi: Ndiyo

Nkoko: Nitakuwa sahihi pia alikuwa amekuamini hata kwa maisha yake maana wewe ndiye ulikuwa unapika chakula?

Shahidi: Ndiyo mimi ndiye nilikuwa napika.

Nkoko: Ndiye uliaminiwa kufanya usafi wa nyumba nzima na mazingira ya nje?

Shahidi: Ndiyo.

Nkoko: Ni kweli kwamba katika maelezo yako hakuna mahali ambapo umeandika kwamba aliyemuua Aneth ni nani?

Shahidi: Sijawahi kusema nani alimuua Aneth.

Nkoko: Kutokana na uhusiano mzuri ulivyoishi na Aneth hukujisikia vibaya kuona ameuawa na ukatoa taarifa za matukio hayo yote?

Shahidi: Sikuweza kutoa taarifa kutokana na vitisho kwa sababu waliniambia kuwa wananifuatilia.

Nkoko: Kwa nini hukumtuma hata Sabri atoe taarifa wa niaba yako, wakati kuna mtu amekufa?

Shahidi: Sikuwa na wazo hilo kwa wakati huo maana baada ya kupata taarifa zilinisikitisha sana.

Nkoko: Kama Mahakama ikiwakuta hawa (washtakiwa) na hatia huoni na wewe utakuwa unahusika kuwasaidia?

Shahidi: Mimi siyo mhalifu ndiyo maana niko hapa.

Nkoko: Hukuhusika kuwasaidia kwa nini tarehs 25 ulitoroka?

Shahidi: Hapana sikuwasaidia

Nkoko: Kama Mahakama ikiamini ulipewa Sh20,000 na ukaahidiwa Sh50 bilioni huoni kama na wewe unahusika kwa kuwa ulitamani (hilo donge nono)?

Shshidi: Mimi sikushiriki kwa sababu hiyo hela walinipa kwa vitisho.

Nkoko: Utakubaliana nani toka tarehe 25 mpaka 28 Mei, 2016 ulikuwa mafichoni Chanika?

Shahidi: Siyo kweli

Nkoko: Ulikuwa wapi tarehe hizo?

Shahidi: Tarehe 25 mpaka 28 nilikuwa nyumbani Masama

Nkoko: Uliondoka lini kwenda Masama?

Shahidi: Tarehe 28/5/2016

Nkoko: Ulipanda basi gani?

Shahidi: Sikumbuki

Nkoko: Ni kweli pale kijijini kuna mlinzi wa amani ambaye unaweza kwenda kumweleza hizo taarifa na akabaki nazo?

Shahidi: Wapo wengi

Nkoko: Sasa una uchungu dada yako kafa kwa nini hukwenda kwa mlinzi wa amani ili hao waliohusika na tukio wakafuatiliwa?

Shahidi: Nilikuwa bado nina hofu ya vitisho.

Nkoko: Hiki ni kielelezo cha Mahakama: Anamuonyesha shahidi Ilani ya Kwanza (taarifa ya awali ya tukio la mauaji ya Aneth), kisha anamuonyesha mahali anamtaka asome jina la mshtakiwa lililoandikwa?

Shahidi: Naomba unisomee

Nkoko: Hapa limeandikwa Getruda Peniel Mfuru, siyo wewe?

Shahidi: Ni mimi.

Nkoko: Dada yako anakaa Gongo la Mboto ipi? maana ni kubwa

Shahidi: Relini

Nkoko: Nyumba ya nani?

Shahidi: Yake mwenyewe

Nkoko: Anakaa na nani?

Shahidi: Na mume wake

Nkoko: Mumewe anaitwa nani?

Shahidi: Simkumbuki

Nkoko: Shemeji yako humkumbuki.

Nkoko: Itajie Mahakama namba za simu ulizokuwa unatumia?

Shahidi: Sizikumbuki.

Nkoko: Namba yako ya sasa hivi itajie Mahakama

Shshidi: Sina kichwani

Nkoko: Nazo huzikumbuki

Shahidi: Sijazikariri kichwani

Nkoko: Ni kweli hukuwahi kuzima simu tangu uliopotoka kwa Aneth mpaka unakwenda Masama?

Shahidi: Sijawahi kuzima simu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live