Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kesi watumishi Jiji D’Salaam ipo hatua ya mwisho

HUKUMU Kesi watumishi Jiji D’Salaam ipo hatua ya mwisho

Thu, 23 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Upande wa mashtaka katika kesi inayowakabili watumishi 15 wa Jiji la Dar es Salaam, umeieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa wapo kwenye hatua ya mwisho kuandaa taarifa ili waipeleke Mahakama Kuu.

Washtakiwa hao wanaotetewa na Wakili Josephat Mabula na Majura Magafu, wanakabiliwa na mashtaka 143 likiwemo la kuisababishia jiji hilo hasara ya zaidi ya Sh8.9 bilioni.

Leo Alhamisi, Novemba 23, 2023, kesi hiyo imetajwa na Wakili wa Serikali, Roida Mwakamele amweeleza Hakimu Mkazi Mkuu, Pamela Mazengo kuwa wapo hatua za mwisho ya kuandaa taarifa ili wazipeleke Mahakama Kuu.

"Tumeshafika kwenye hatua ya mwisho ya uandaaji wa taarifa, hivyo naiomba Mahakama ipange tarehe nyingine ya kutajwa," amedai Mwakamele.

Baada ya maelezo hayo, Pamela ameahirisha kesi hadi Desemba 21, 2023.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni Tulusubya Kamalamo na James Bangi ambayo ni wahazini, Mohamed Khars, Abdallah Mlwale na Deogratias Lutatuza ambao ni wahasibu na Judica Ngowo ambaye ni karani wa fedha.

Wengine ni Febronia Nagwa, Glory Eugen, Said Bakari, Josephine Sandewa, Dorica Gwihala, Jesca Lugonzibwa, Patrick Chibwana ambao ni wahasibu, Patrick Chubwana ni Ofisa Afya, Ally Baruan ambaye ni meneja na Khalid Nyakamande, ofisa mtendaji wa mtaa.

Katika kesi hiyo wanadaiwa tarehe tofauti kati ya Julai mosi, 2019 hadi Juni 30, 2021, waliongoza genge la uhalifu na kujipatia Sh8.93 bilioni, mali ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.

Pia washhtakiwa hao wanakabiliwa na shtaka la matumizi mabaya ya madaraka, kwa kushindwa kuingiza malipo ya watu mbalimbali katika akaunti za jiji hilo zilizo Benki ya NMB, NBC, CRDB na DCB.

Mshtakiwa Judica, Febronia, Bakari na Glory wanakabiliwa na mashtaka 53 ya kuingiza taarifa za udanganyifu katika mfumo wa malipo kwa lengo la kuonyesha malipo ya watu mbalimbali yaliingizwa katika akaunti za jiji hilo wakati wakijua si kweli.

Inadaiwa washtakiwa Dorica, Chibwana, Baruani na Nyakamande wakiwa wahasibu, wahazini wanakabiliwa na mashtaka ya ubadhirifu wa Sh8.93 bilioni kwa kuzitumia kwa matumizi yao binafsi.

Pia, inadaiwa tarehe hizo mshtakiwa Kamalamo, Bangu, Sandewa, Gwihala, Lugonzibwa, Chibwana, Baruan na Nyakamande wanakabiliwa na mashtaka ya kugushi nyaraka mbalimbali wakijifanya ni halisi, wakati wakijua si kweli.

Iliendelea kudaiwa washtakiwa hao pia wanakabiliwa na shtaka la kuisababishia hasara ya zaidi ya Sh8.93 bilioni.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live