Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kesi washitakiwa wa meno ya tembo ya Sh1.466 bilioni Juni 11 na 12

60024 PIC+MENO

Tue, 28 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi, imepanga siku mbili mfululizo kuanza kusikiliza ushahidi katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili, Mohamed Mboweto (42)  maarufu Ustadhi na wenzake saba.

Mboweto ambaye ni mkazi wa Mbagala Kiburugwa na wenzake, wanakabiliwa na mashtaka manne, la kujihusisha na biashara haramu ya meno ya tembo yenye thamani ya Sh1.466bilioni.

Uamuzi huo umetolewa leo, Mei 27, 2019 na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Huruma Shaidi baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) kuipa mamlaka Mahakama ya Kisutu kusikiliza kesi hiyo.

Hakimu Shaidi alisema kutokana na kesi hiyo kuwa ya muda mrefu, mahakama yake imepanga Juni 11 na 12, 2019 kuanza kusikiliza ushahidi wa upande wa mashtaka.

Kwa kawaida kesi za uhujumu uchumi huwa zinasikilizwa Mahakama Kuu, Kitengo cha Rushwa na Uhujumu Uchumi, lakini DPP akiona inafaa kulingana na mazingira anaweza kutoa hati ya kuipa Mamlaka, Mahakama ya chini kusikiliza kesi hizo.

Awali, wakili wa Serikali Elizabeth Mkunde alidai kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kuanza kusikiliza lakini wamepata changamoto katika uletaji wa vielelezo.

Pia Soma

“Kesi imekuja kwa ajili ya kuanza kusikiliza ushahidi wa upande wa mashtaka, lakini kwa bahati mbaya tumepata changamoto katika uletaji wa vielelezo,” alidai Mkunde.

Mkunde baada ya kueleza hayo, hakimu Shaidi aliahirisha kesi hiyo hadi Juni 11, itakapoanza kusikilizwa na washtakiwa wote wamerudishwa rumande kutokana na mashtaka yanayowakabili kutokuwa na dhamana.

Mbali na Mboweto, washtakiwa wengine katika hiyo ya uhujumu uchumi namba 4/2016 ni Robert Mwaipyana (32) mkazi wa Mabibo; Ramadhani Mnekea (55) dereva na mkazi wa Temeke; Ramadhan Matimbwa (42).

Wengine ni Exavery Silvester(36) dereva na mkazi wa Masasi mkoani Mtwara; Frank Sadik (51) mkazi wa Mtwara; Issa Pilla (43) mfanyabiashara na mkazi wa Masasi na Cliford Maivaji (51) mfanyabiashara na mkazi wa Temeke.

Washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka manne, likiwamo la  kujihusisha na mtandao wa ujangili.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa wanadaiwa kati ya Januari Mosi, 2015 na Desemba 21, 2015, katika maeneo ya Dar es Salaam na Mtwara, walijihusisha na mtandao wa ujangili kwa kukusanya na kuuza vipande 161 vya meno ya tembo.

Alidai vipande hivyo vina  uzito wa kg 220.96 na vina  thamani ya dola za Marekani 690,000, ambazo ni sawa na Sh1,466,250,000, mali ya Serikali ya Tanzania na kwamba washtakiwa hao walikuta na nyara hizo, bila kuwa na kibali  cha Mkurugenzi wa Wanyama Pori nchini.

 

 

Chanzo: mwananchi.co.tz