Dar es Salaam. Mahakama ya Wilaya ya Ilala Julai 22 ,2019 itaanza kusikiliza kesi ya kuomba rushwa inayowakabili viongozi watatu wa CCM.
Viongozi hao wanadaiwa kuomba rushwa ya Sh5 milioni na kupokea Sh3 milioni.
Watuhumiwa ni Katibu wa CCM tawi la Amana, Jenifer Mushi (47); Katibu Kata Ilala, Devotha Batulake (43) na Katibu Uhamasishaji Mkoa wa Dar es Salaam, Frank Mang'ati (38).
Uamuzi huo wa mahakama umekuja baada ya wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Veronica Chimwada kueleza kuwa wanatarajia kuwaita mashahidi saba wa upande wa mashtaka kutoa ushahidi kwenye kesi hiyo na vielelezo visivyopungua vinne.
Hatua hiyo imekuja baada ya upande wa mashtaka kukamilisha upelelezi na washtakiwa hao kusomewa maelezo ya awali mbele ya hakimu mfawidhi, Martha Mpaze.
Wakisomewa maelezo hayo ya awali washtakiwa wote walikubali maelezo yao binafsi ikiwamo shughuli wanazozifanya ndani ya CCM.
Pia Soma
- Kesi ya Kitilya sasa yaiva Mahakama ya Ufisadi
- Waziri Mhagama: Watanzania changamkieni fursa bomba la mafuta
- RC awataka wananchi kujitokeza kumpokea Rais Kenyatta
- Mali za Mbowe kupigwa mnada
Katika kesi hiyo ya jinai namba 250 ya mwaka 2019 washtakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kuwa Machi 21,2019 katika klabu ya wazee Amana walishawishi rushwa ya Sh5 milioni kutoka kwa mmiliki wa kampuni ya Daluni East Africa Transport, Daud Kalaghe ili waweze kumpatia kiwanja namba 41 Y kinachomilikiwa na CCM kwa shughuli ya biashara.
Inadaiwa kuwa Machi 22, 2019 katika eneo la Msimbazi Sekondari washtakiwa hao walijipatia rushwa ya Sh3 milioni kutoka kwa Kalaghe ili waweze kumpatia kiwanja namba 41 Y kinachomilikiwa na CCM kwa shughuli ya biashara.
Washtakiwa hao wapo nje kwa dhamana baada ya kukamilisha masharti ya kila mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili.
Washtakiwa hao walikamatwa Machi 21, 2019 baada ya kuwekewa mtego na Takukuru.