Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kesi vigogo TRL kusikilizwa mfululizo

Thu, 30 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imepanga kusikiliza ushahidi wa kesi ya vigogo 18 wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) kwa siku mbili mfululizo.

Leo Alhamisi Mei 30, 2019 wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Maghela Ndimbo amewasomea hoja za awali washtakiwa hao mbele ya Hakimu Mkazi mfawidhi, Kelvin Mhina na kudai shauri hilo litasikilizwa Julai 3 na 4, 2019.

Vigogo hao ni aliyekuwa mkurugenzi mtendaji wa TRL, Kipallo Kisamfu; mkuu wa kitengo cha makenika na mhasibu mkuu, Jasper Kisiraga; kaimu meneja wa usafiri, Mathias Massae; kaimu mhandisi wa ufundi na meneja ujenzi, Muungano Kaupunda na mkuu wa ufundi na meneja ujenzi, Ngoso Ngosomwiles.

Wengine ni mhandisi mkuu wa ufundi, Paschal Mafikiri;  mhandisi mipango,  Kedmo Mapunda;  kaimu mhandisi wa mawasiliano, Felix Kashaingili; mkuu wa usafiri wa reli, Lowland Simtengu; mkuu wa ubunifu na utengenezaji wa nyaraka, Joseph Syaizyagi na kaimu mkuu wa usafirishaji, Charles Ndenge.

Awali, walisomewa mashtaka yanayowakabili na wote walikana kuhusika, ndipo wakasomewa maelezo ya kesi namna walivyohusika kutenda makosa na makosa  wanayotuhumiwa.

Baada ya kusomewa maelezo hayo  walitakiwa kubainisha mambo wanayokubaliana na wasiokubaliana.

Pia Soma

Hata hivyo, Kisamfu amekana maelezo ya kesi isipokuwa jina lake na wadhifa wake na washtakiwa wengine wamekubali majina yao huku wakikataa maelezo yote na nyadhifa zao.

Baada ya kusomewa maelezo ya awali washitakiwa hao walipewa nakala za hoja kwa ajili ya kuzipitia wakishirikiana na mawakili wao.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Julai 3 na Julai 4, 2019.

Katika hati ya mashtaka inadaiwa kuwa kati ya Februari Mosi,  2013 na Juni 30, 2014 makao makuu ya TRL, Kisamfu akiwa mfanyakazi wa mamlaka hiyo, alitumia vibaya madaraka yake kwa kushindwa kusimamia vizuri zabuni kama ilivyokuwa inatakiwa kwenye vigezo na masharti.

Inadaiwa kuwa tukio hilo ni kinyume cha sheria namba 21 ya manunuzi ya 2004 jambo lililoipa faida kampuni ya M/S Hindusthan Engineering and Industries Limited.

Upande wa Jamhuri ulidai kuwa kati ya Julai Mosi na Agosti 31, 2013, Mafikiri alitumia madaraka yake vibaya kwa kuidhinisha michoro iliyoandaliwa na M/S Hindusthan jambo ambalo ni kinyume cha vigezo na masharti ya zabuni.

Pia, Kaupunda anadaiwa alitumia madaraka vibaya kwa kuruhusu kutengenezwa kwa mabehewa 25 bila kuzingatia vigezo na masharti ya zabuni hiyo.

Katika mashitaka mengine, Kisiraga na Massae wanadaiwa Agosti 5, 2014, walitumia madaraka vibaya kwa kuidhinisha malipo ya Dola 1.3milioni za Marekani bila kuthibitisha matumizi ya mabehewa 25, kupitia cheti cha ukaguzi na cha kukubali kinachotolewa na TRL baada ya kufanyiwa majaribio jambo ambalo ni kinyume cha sheria na kanuni za manunuzi.

Inadaiwa kati ya Januari Mosi na Februari 2014, washtakiwa Kaupunda, Mapunda, Kashaigili, Simtengu na Syaizyagi, wakiwa wajumbe wa bodi ya zabuni, walitumia madaraka yao vibaya kwa kuiruhusu M/S Hindusthan kushinda, ambayo ilikuwa haijakidhi vigezo kushinda zabuni hiyo.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz