Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kesi polisi wanaodaiwa kuua Mtwara yaahirishwa mara 11

3d49727d27c27864869e2531a9e09747.png Kesi polisi wanaodaiwa kuua Mtwara yaahirishwa mara 11

Fri, 17 Jun 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kesi ya mauaji inayowakabili maofisa saba wa Jeshi la Polisi mkoani Mtwara imeahirishwa kwa mara ya 11 na itatajwa tena Juni 29, mwaka huu. Kesi hiyo ipo chini ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mtwara, Lugano Kasebele.

Maofisa hao wa polisi walifikishwa mahakamani hapo jana wakidaiwa kufanya mauaji hivi karibuni ya mfanyabiashara wa madini, Mussa Hamisi (25) mkazi wa Kijiji cha Ruponda, Wilaya ya Nachingwea, mkoani Lindi. Kesi hiyo ilitajwa kwa njia ya mtandao ikiwa ni mara ya pili kutajwa kwa njia hiyo na utaratibu huo sasa utakuwa endelevu.

Washtakiwa hao jana ni mara ya 11 kufikishwa mahakamani hapo, ambapo mara ya kwanza walifikishwa Januari 25, mwaka huu, mara ya pili Februari 8, mara ya tatu Februari 22, mara ya nne Machi 8 na mara ya tano ni Machi 22, mwaka huu. Mara ya sita kuahirishwa ilikuwa Aprili 5, mara ya saba Aprili 19, mara ya nane Mei 10, mara ya tisa Mei 23, mara ya 10 Juni 6 na mara 11 ni jana, Juni 16.

Kesi hiyo namba moja ya mauaji kwa mwaka 2021/22, inaendeshwa na Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Severine Mganga. Inadaiwa mauaji hayo yalifanyika baada ya mfanyabiashara huyo kudai fedha zake Sh 33,748,980 ambazo maofisa hao wa Jeshi la Polisi wanadaiwa kuzichukua kutoka kwake wakati walipomfanyia upekuzi.

Washitakiwa hao ni Mrakibu wa Polisi, Gilbert Kalanje ambaye ni Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Mtwara, Mrakibu Msaidizi wa Polisi, Charles Onyango ambaye ni Mkuu wa Kituo cha Polisi Mtwara na Mrakibu wa Polisi Msaidizi, Nicholaus Kisinza ambaye ni Mkuu wa Kikosi cha Intelijensia ya Jinai Mkoa wa Mtwara.

Wengine ni Mkaguzi wa Polisi, John Msuya ambaye ni Mganga Mkuu wa Zahanati ya Polisi mkoani Mtwara, Mkaguzi wa Polisi Msaidizi, Marco Mbuta, Mkaguzi wa Polisi, Shirazi Mkupa na Koplo Salimu Mbalu. Mauaji hayo yalifanyika Januari 5, mwaka huu na mwili wa mfanyabiashara huyo ulikutwa umetupwa katika Kitongoji cha Majengo, Kijiji cha Hiari Wilaya ya Mtwara.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live