Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kesi nyingine ya ‘Mfalme Zumaridi’ na wenzake 84 yapigwa kalenda

Zumaridi Vv Zumaridi anakabiliwa na kesi kadhaa za kujibu

Thu, 12 May 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza imeahirisha kesi namba 10 inayomkabili Diana Bundala maarufu kama 'Mfalme Zumaridi' na kesi namba 12 inayomkabili mhubiri huyo na wenzake 84 ili kupisha usikilizwaji wa shauri lingine la mauaji.

Katika shauri namba 10, Mfalme Zumaridi anakabiliwa na shtaka la kufanya usafirishaji haramu wa binadamu huku katika shauri namba 12, mhubiri huyo na wenzake 84 wanakabiliwa na shtaka la kufanya kusanyiko lisilo na kibali.

Katika mashauri hayo upande wa Jamhuri unawakilishwa na Mawakili wa Serikali waandamizi, Emmanuel Luvinga na Dorcas Akyoo na wakili wa Serikali, Deogratius Lumanyika huku upande wa utetezi ukiwakilishwa na Wakili, Erick Mutta.

Baada ya washtakiwa kusomwa majina yao, wakili Luvinga aliiambia mahakama hiyo kuwa upelelezi katika shauri namba 10 linalomkabili Mfalme Zumaridi peke yake haujakamilika huku shauri namba 12 upelelezi wake ukiwa umekamilika na kuomba ruhusa kwa ajili ya kuwasomea washtakiwa maelekezo ya awali.

Wakati huo wakili wa utetezi, Erick Mutta akaiomba mahakama hiyo kutoa amri kwa upande wa Jamhuri kukamilisha upelelezi wa shauri namba 10 ili lianze kutajwa kwani zimepita zaidi ya siku 60 tangu shauri hilo lifikishwe mahakamani hapo bila upelelezi wake kukamilika.

Baada ya maombi hayo, Hakimu Mkazi Mwandamizi wa mahakama hiyo, Monica Ndyekobora akahairisha mashauri hayo hadi Mei 24, 2022 kwa lengo la kupisha usikilizwaji wa mashauri ya mauaji yanayotakiwa kusikilizwa ndani ya mahakama hiyo.

Advertisement "Washtakiwa walioko rumande wataendelea kukaa huko hadi tarehe ya kutajwa tena mashauri yao," amesema Ndyekobora

Chanzo: www.tanzaniaweb.live