Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kesi nne kuunguruma kesho, ikiwemo ya Halima Mdee

40482 Pic+mdee Kesi nne kuunguruma kesho, ikiwemo ya Halima Mdee

Thu, 7 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar Es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kesho Alhamisi  Februari 7, 2019 itaendele kusikiliza ushahidi katika kesi ya kutoa lugha chafu dhidi ya Rais John Magufuli inayomkabili mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee.

Kesi hiyo itasikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

Tayari mashahidi watatu wa upande wa mashtaka wamekwishatoa ushahidi dhidi ya mshtakiwa huyo, akiwamo  mkuu wa kituo cha polisi cha Urafiki, mrakibu wa Polisi (SP),  Batseba Kasanga.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, inadaiwa kuwa Julai 3,2017  katika ofisi za makao makuu ya Chadema mtaa wa Ufipa Wilaya ya Kinondoni, Mdee anadaiwa kutamka maneno dhidi ya  Rais  Magufuli kuwa, “anaongea hovyohovyo , anatakiwa  afungwe breki”  kitendo ambacho kingeweza  kusababisha uvunjifu wa amani.

Hata hivyo, Mdee alifikishwa kwa mara ya kwanza Kisutu, Julai 10, 2017 kujubu shtaka hilo.

 

Wakati huo huo, kesi ya uhujumu uchumi na kuisababishia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) hasara ya Sh188.9 bilioni inayomkabili Mustapha Kambangwa (34), itatajwa.

 

Kambangwa ambaye ni mfanyabiashara na mkazi wa Mbagala Kongowe,  anakabiliwa na mashtaka manne likiwemo la utakatishaji  wa fedha.

 

Kesi hiyo inasikilizwa mbele ya hakimu Mkazi, Janeth Mtega.

 

Kambangwa alifikishwa kwa mara ya kwanza Kisutu,  Desemba 7, 2018 na kusomewa mashitaka yake katika kesi ya uhujumu uchumi namba 19/ 2018 .

 

Inadaiwa mshtakiwa anakabiliwa na mashitaka manne aliyoyatenda katika siku tofauti kati ya Juni Mosi ,2016 na Novemba 2, 2018.

 

Miongoni mwa mashtaka hayo, Kambangwa anadaiwa  katika tarehe tofauti kati ya Juni Mosi, 2016 na Novemba 2, 2018, maeneo ya jiji la Dar es Salaam alijifanya kuwa amesajiliwa kukusanya kodi ya VAT kiasi  cha Sh 188,928,752,166, kwa kujifanya anakusanya fedha hizo kwa niaba ya TRA.

 

Katika hatua nyingine, kesi ya ya Uhujumu Uchumi inayomkabili mfanyakazi mstaafu wa Shirika la Mafuta Tanzania na Zambia(Tazama), Samwel Nyakirang'ani (63) na wenzake 11, itatajwa katika mahakama hiyo.

Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa Kisutu, Januari 16, 2018 kujibu mashtaka matatu likiwemo la kujiunganishia isivyo halali bomba la mafuta, mali ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA),  lakini hadi sasa upelelezi wake bado haujakamilika.

Mbali Samweli, washtakiwa wengine katika kesi  hiyo namba 1/2018 ni Nyangi Mataro( 54) mwalimu wa shule ya  msingi Ufukoni na mkazi wa Kisiwani Mkajuni Kigamboni.

Mfanyabiashara, Farijia Ahmed(39) mkazi wa Soko Maziwa Kigamboni; Malaki Mathias(39) mkazi wa Magogoni;  Kristomsi Angelus(25) mkazi wa Soko Maziwa; fundi ujenzi, Pamfili Nkoronko(40) mkazi wa Tungi Kasirati na Henry Fredrick (38) mkazi wa Tungi Kigamboni.

Wengine ni Audai Ismail (43) mkazi wa Kibaha;  Chibony Emmanuel, Roman Abdon, Amina Shaban na Zubery Ally.

Kwa pamoja wanadaiwa kati ya mwaka 2015 hadi Januari 8, 2018 katika eneo la Tungi Muungano wilaya ya Kigamboni, wanadaiwa kujiunganishia bomba la mafuta ya dizeli lenye upana wa inchi moja kutoka katika bomba lenye upana wa inchi 24, bila kuwa na kibali.

Pia , kesi ya utakatishaji fedha, inaomkabili, Mhasibu wa Ubalozi wa Tanzania nchini Msumbiji, Joyce Mushi (56), itatajwa mahakamani hapo.

Mushi ambaye ni mkazi wa Temeke, anakabiliwa na mashtaka ya kughushi, kuwasilisha nyaraka za kughushi, wizi akiwa mtumishi wa umma na utakatishaji wa fedha.

Katika kesi hiyo ya jinai namba  340/2017,  Joyce anadaiwa kuwa  Oktoba 25, 2016 katika ofisi za ubalozi wa Tanzania zilizopo Maputo nchini Msumbiji, mshtakiwa alighushi barua, akijaribu kuonyesha kuwa ofisi ya ubalozi umeilekeza Benki ya Millennium (BIM) ya Maputo, kuhamisha Dola 10,000 za Marekani kutoka kwenye akaunti namba 79667362 kwenda akaunti namba 182283177 inayomilikiwa na Mushi.



Chanzo: mwananchi.co.tz