Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kesi mume anayedaiwa kughushi saini ya mkewe kuunguruma Januari

Kortiiiiiii Pic Kesi mume anayedaiwa kughushi saini ya mkewe kuunguruma Januari

Wed, 28 Dec 2022 Chanzo: Mwananchi

Mashahidi sita na vielelezo sita, vinatarajia kutolewa katika kesi ya kughushi ridhaa na siani ya mke wake na kisha kujipatia mkopo wa Sh 140 milioni kwa njia ya udanganyifu, inayomkabili mfanyabiashara Seleman Maziku.

Maziku, mkazi Kitunda Mwanagati wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam anadaiwa kujipatia kiasi hicho cha mkopo kutoka benki ya Stanbic, baada ya kuwasilisha nyaraka ya kughushi ikionyesha mke wake Schola Bundala ametoa ridhaa kwa mume wake kuchukua mkopo huo katika benki hiyo.

Wakili wa Serikali, Caroline Matemu ameieleza mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, leo Jumatano Desemba 28, 2022 wakati akimsomea maelezo ya awali( PH) mshtakiwa huyo, baada ya upelelezi wake kukamilika.

Kabla ya kumsomea maelezo yake, wakili Matemu alimkumbusha mshtakiwa mashtaka yanayomkabili.

Akimsomea maelezo hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Mary Mrio, wakili Matemu amedai mshtakiwa anakabiliwa na kesi ya jinai namba 200/2022 yenye mashtaka ya kughushi na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Wakili Matemu amedai Mahakamani hapo Seleman alikuwa akiishi na mkewe katika nyumba ya familia eneo la Mwanagati.

Inadaiwa siku ya tukio, Desemba 10, 2022 katika eneo lisilojulikana jijini Dar es Salaam, mshtakiwa bila ya ridhaa kutoka kwa mke wake alisaini nyaraka ya mkopo akionyesha kuwa imesainiwa na Schola.

Maziku baada ya kusaini nyaraka hiyo, aliiwasilisha benki ya Stanbic kama moja ya taratibu za kibenki zinavyotaka, kitendo kilichosababisha mshtakiwa alijipatia mkopo wa Sh 140milioni uliotolewa na benki hiyo, wakati akijua kuwa nyaraka hiyo ameghushi na haijaridhiwa na mke wake.

Wakili Matemu aliendelea kuieleza mahakama hiyo kuwa Desemba 18, 2022 Schola aligundua kuwa mume wake ameghushi saini yake na kwenda kutoa taarifa kituo cha Polisi na baadaye Maziku alikamatwa kwa ajili ya kuhojiwa.

Mshtakiwa baada ya kukamatwa alichukuliwa Sampuli za maandishi ikiwemo saini yake aliyoiweka na kushuhudiwa na wakili Castor Rwekiza pamoja na saini ya Schola na kisha kupelekwa katika maabara kwa ajili ya uchunguzi.

Hata hivyo, uchunguzi ulibaini kuwa saini iliyowekwa katika nyaraka hizo iliwekwa na mshtakiwa na sio mke wake.

Baada ya kukamalika uchunguzi wa awali wa polisi, mshitakiwa alifikishwa Mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.

Mshtakiwa huyo, ambaye anatetewa na wakili Peter Shapa, baada ya kusomewa mashtaka pamoja na maelezo yake, alikana tuhuma zinazomkabili huku akikiri majina yake na siku alipofikishwa mahakamani.

Hakimu Mrio baada ya kusikiliza maelezo hayo, ameahirisha kesi hiyo hadi Januari 23, 2023 itakapoanza kusikilizwa ushahidi wa upande wa mashtaka.

Hata hivyo, mshtakiwa yupo nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti yaliyomtaka awe na wadhamin wawili wanaotambuliwa kisheria watakao wasilisha hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya Sh 70milioni.

Chanzo: Mwananchi