Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kesi mke wa bilionea Msuya: RCO katika mzani wa Wakili Kibatala

Msuya Bilionea.jpeg Mkuu wa wapelelezi katika mzani wa Wakili Kibatala

Fri, 1 Sep 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kesi ya mjane wa Bilionea Msuya jana iliahirishwa mpaka Jumatatu, kutokana na wazee wa Baraza katika kesi hiyo kuhudhuria katika kesi nyingine. Kabla ya kuahirishwa shahidi wa 22 alikuwa katika mchuano mkali na wakili wa utetezi Peter Kibatala. Leo hii tutaona sehemu ya pili ya mahojiano hayo.

Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Arusha (RCO), Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) David Paulo Mhanaya, ni shahidi wa 22 wa upande wa mashtaka katika kesi ya mauaji Aneth Msuya.

Aneth alikuwa mdogo wa aliyekuwa mfanyabiashara tajiri maarufu wa madini mkoani Arusha, marehemu Erasto Msuya, maarufu kama Bilionea Msuya, aliyeuawa kwa kupigwa risasi eneo la Mijohoroni, wilayani Hai mkoani Kilimanjaro Agosti 7, 2013.

Aliuawa Mei 26, 2016 kwa kuchinjwa nyumbani kwake Kibada, Kigamboni, wilayani Temeke (wakati huo), jijini Dar es Salaam, na mwili wake ulikutwa ndani ya nyumba yake ukiwa uchi na nguo yake ya ndani ikiwa pembeni ya mwili huo.

Washtakiwa katika kesi hiyo namba 103/2018 inayosikilizwa na Jaji Edwin Kakolaki ni Miriam Steven Mrita, ambaye ni mjane wa Bilionea Msuya, na mwenzake Muyalla.

Kesi hiyo inaendelea kusikilizwa ushahidi wa upande wa mashtaka.

SSP Mhanaya alikuwa kiongozi wa tiny ya upelelezi wa mauaji hayo iliyoteuliwa na aliyekuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Mkosa ya Jinai (DCI), Diwani Athumani Msuya wakati huo, baada ya kutoridhishwa na jinai upelelezi wa awali ulivyokuwa ikiendelea.

Katika ushahidi wake akiongozwa na mwendesha mashtaka Wakili wa Serikali Mwandamizi, Paul Kimweri shahidi huyo alieleza mahakama yale aliyoelezwa na aliyekuwa binti wa kazi wa marehemu Aneth; Getruda Peniel Mfuru, kuhusu matukio kabla ya mauaji ya mwajiri wake.

Aliieleza mahakama jinsi walivyoyafanyia kazi maelezo ya binti huyo wa kazi wa marehemu Aneth hadi wakawakamata washtakiwa jijini Arusha kwa nyakati tofauti na yale washtakiwa waliyoyaeleza baada ya kukamatwa na kuhojiwa

Maswali ya dodoso

Baada ya kuhitimisha ushahidi wake mkuu, akiongozwa na mwendesha.mashtaka, shahidi alihojiwa maswali ya dodoso na Wakili wa utetezi Peter Kibatala kuhusiana na ushahidi wake wote alioutoa kwa siku tatu, Kwa lengo la kuutikisa ili kuona uimara wake.

Ifuatavyo ni sehemu ya pili ya sehemu ya mahojiano hayo aina yake na Wakili Kibatala:

Kibatala: Kwa ufahamu wako huyu Getruda alipokamatwa huko.alifanyiwa upekuzi?

Shahidi: Mheshimiwa Jaji anayefanyiwa upekuzi ni mtuhumiwa.

Kibatala: Alifanyiwa?

Shahidi: Hakufanyiwa

Kibatala: Ulipomfanyia mahojiano ulijiridhisha kuwa.alikuwa na simu au hakuwa nayo?

Shahidi: Hakuwa na simu

Kibatala: Getruda akikusimilia kuwa alikuwa na simu na alipewa na washtakiwa na akaambiwa aitupe baharini, hii ni taarifa kutoka kwa mtu anaweza hata akadanganya. Hii taarifa wewe ulii-verify (uliithibitisha) vipi?

Shahidi: Tuli-verify

Kibatala: Mli-verify vipi?

Shahidi: Tuliwakabidhi wenzetu wa cybercrime

Kibatala: Wewe ulii-verify vipi?

Shahidi: Tulikwenda naye hadi Feri akatuambia kuwa alitumbukiza hapa.

Kibatala: Wewe kama senior Police officer (afisa wa Polisi Mwandamizi) una taarifa nyingine ya kisayansi kwamba simu ilitumbukizwa hapo?

Shahidi: Tuliongea na wenzetu wa Temesa (Wakala wa Ufundi na Umeme) wakasema simu ilitumbukizwa hapo bahari haiwezi kutunza kitu inaweza kutokea hata Comoro.

Kibatala: Kwa hiyo kwa ufupi hakuna.

Shahidi: Kimya

Kibatala: Shahidi kwa ushahidi tulio nao hapa, chumbani kwa marehemu Aneth uliweza kufahamu iwapo chumba cha marehemu kilikuwa na fedha.na mali nyingine na zilienda wapi?

Shahidi: Sikufahamu

Kibatala: Uliweza kuchunguza iwapo marehemu Aneth Msuya alikuwa na ugomvi na watu wengine kazini au sehemu yoyote?

Shahidi: Tuliweza kuwahoji watu mbalimbali lakini hatukuweza kubaini

Kibatala: Ulimhoji nani na nani kazini kwa marehemu?

Shahidi: Tuliwahoji watu mbalimbali hatukunaini

Jaji: Umeelewa Swali Lake?

Shahidi: Ndio

Kibatala: Sasa mlimhoji nani na nani kazini kwa Aneth?

Shahidi: Mimi binafsi sikumhoji mtu yeyote.

Kibatala: Unafahamu kama Aneth alikuwa na mtoto wa miaka.minne?

Shahidi: Ndio

Kibatala: Ulimwambia Jaji kuwa mlipata kumhoji huyo mtoto?

Shahidi: huyo mtoto nilimzunhumzia kwenye maelezo yangu.

Kibatala: Mlimhoji?

Shahidi: Sikumbuki

Kibatala: Sasa tukio lilifanyika ndani ya nyumba na mlisimuliwa na Getruda ambaye hakuwepo, Mlimhoji yule mtoto maana mtoto wa miaka minne anaweza kueleza mambo.

Shahidi: Mheshimiwa Jaji hilo hakikufanyika kwa sababu yule.mtoto alikuwa amelala, alipoamka ndipo akamuamsha mama yake bila kuamka akaenda Kwa mama muuza vitumbua akawambia anamuamsha mama yake haamuki na amechafuka.

Kibatala: Huyo mama muuza vitumbua wewe ulimhoji?

Shahidi: Sikumhoji

Kibatala: Unajua maana ya hearsay? Maana nikilisikia jana unataja vifungu vya sheria?

Shahidi: Unamaana ushahidi wa kusikia?

Kibatala: Mimi sijui

Kibatala: Wewe unamfahamu hata jina huyo mama muuza vitumbua?

Shahidi: Mheshimiwa Jaji Wakili ananiuuliza mambo ambayo sikuwepo

Jaji: Shahidi umeulizwa unamfahamu?

Shahidi: Simfahamu

Kibatala: Kwa taarifa zako mwili wa marehemu ulikutwa wapi?

Shahidi: Kwenye korido

Kibatala: Ahaa, hiyo ni new facts (taarifa mpya). Sasa soma hii document (Anampatia nyaraka)

Shahidi: Kwanza hii document nimeshaikataa tangu mwanzo.

Kibatala: Shahidi hii ni document ya Mahakama nimeiomba Mahakamani huwezi kuikataa. Kwa mujibu wa document hiyo mwili wa marehemu ulikutwa wapi? Soma hiyo document

Shahidi: Nimesema hii nimeikataa tangu awali.

Jaji: Shahidi wewe jibu swali

Shahidi: Anasoma...mwili wa marehemu ulikutwa chumba cha watoto ukiwa umelala sakafuni ukiwa uchi.

Kibatala: Shahidi umitumwa kwenda kufanya uchunguzi zaidi, DCI alikuwa hajaridhika, ulimuuliza muuza duka kama aliona gari ya Ford Rangers Getruda akiongea na mtu siku hiyo (aliyoitaja shahidi)?

Shahidi: Sikuona umuhimu maana dukani ni mbali (kutoka alikokuwa akiishi marehemu Aneth.

Kibatala: Unafahamu au hufahamu kwamba mshtakiwa wa kwanza ameleta deffence ya alibi ( utetezi wa kutokuwepo eneo la tukio?

Shahidi: Mimi Sifahamu

Kibatala: Unafahamu kwamba moja ya majukumu.yako ni kuthibitisha kuwa tarehe 15/5/2016 (mshtakiwa wa kwanza Miriam) alikuwepo Dar kufanya maandalizi?

Shahidi: Wala haina shida Mheshimiwa Jaji suala.la kuthibitisha lilo maana kuna mashahidi mbalimbali Tuliwahoji.

Jaji: Shahidi: Shahidi uwe unasikiliza swali, anakuuliza wewe unafahamu?

Shàhidi: Ndio Mheshimiwa Jaji

Kibatala: Hilo gari la Ford Ranger wewe kama.mpelelezi Unafahamu limesajiliwa kwa jina la nani?

Shahidi: Sikumbuki mheshimiwa Jaji

Kibatala: Unafahamu kuwa gari hilo lilipelekwa CMC Cooper Motors Company Kwa matengenezo?

Shahidi: Sifahamu

Kibatala:Na wewe mpelelezi... huyu mshtakiwa wa kwanza alifikia hoteli gani Dar?

Shahidi: De France Hotel

Kibatala: Ambako kuna CCTV camera, siyo?

Shahidi: Ndio lakini storage (uwezo wa kuhifadhi taarifa) yake ni ndogo.

Kibatala: Kwa hiyo hatuwezi kupata taarifa kuwa washtakiwa walifika hapo na gari gani kwa kuwa storage ya CCTV ni ndogo?

Shahidi: ndio hatuwezi kupata footage (video) za picha lakini mashahidi wapo waliompokea na wanaweza kueleza walimpa chumba gani

Kibatala: Sawa, kama wapo kwenye orodha tutawauliza. Wakati unaongozwa ulimwambia Jaji kwamba kuna shahidi aliyewapokea?

Shahidi: Watakuja kuizungumzia wengine.

Kibatala: Huyo shahidi aliyewapokea ni wewe uliyemhoji?

Shahidi: Ni wapelelezi wenzangu.

Kibatala: Ulipokwenda kumpekuw mshtakiwa wa kwanza uliwahi kuwauliza ndugu au watoto wake au housegirl kujiridhisha kama.tarehw hiyo hakuwepo alikuwa Dar?

Shahidi: Sikuona sababu hao ni ndugu wangeweza kumlinda.

Kibata: Shahidi wewe ndio uliji-introduce kwenye record kwamba ulifundishwa na FBI, Unafahamu kwa nini hizo taasisi huwa zinafanya upelelezi kwa muda mrefu?

Shahidi: Sijui unataka ku-achieve nini maana siwezi kuizungumzia taasisi ya Nchi nyingine.

Kibatala: Ni wewe uliyetaja na huwezi kunipangia maswali

Jaji: Shahidi, nimeshakwambia wewe jibu kama unavyoulizwa Unafahamu au hufahamu?

Kibatala: Kwa nini huwa wanavhukua muda mrefu miaka mitatu au zaidi kupeleleza kesi badala ya ku- rush?

Shahidi: Kwa sababu wanahitaji umakini

Kibatala: Sasa shahidi hapo (namna yeyeh alivyofanya upelelezi) kuna umakini?

Shahidi: Usinifundishe Wakili Msomi

Kibatala: Shahidi sijakufundisha ni wewe umetaja kuwa ni kuwa na umakini, sasa nakuuliza kuna umakini hapo?

Shahidi: Wakati mwingine kunakuwa na umakini.

Kibatala: Shahidi nilisikia ukisema kuwa Getruda alimsikia mshtakiwa wa kwanza akisema kuwa mali nitafute mimi watumie wengine kama mpelelezi hayo yalimaanisha nini?

Shahidi: Hii inaonesha jinsi mshtakiwa alivyokuwa na chuki ya mali na kwa marehemu Aneth na inatbibitishwa na mshtakiwa alishaanza kuuza Mali.

Kibatala: Ni mali zipi ambazo mshtakiwa alianza kuziuza?

Shahidi: Kuna magari ambayo sisi tulikuwa tumeya- seize (tumeyakamata) yaliahaanza kuuzwa na kubadilishwa.

Kibatala: Gari gani namba gani?

Shahidi: Nitataja moja mfano Toyota Land Cruiser.

Kibatala: Mwambie Jaji umiliki wa awali ulikuwa ni kwa nani na ililibadilishwa kutoka kwa nani kwenda kwa nani?

Kibatala: Kutoka kwa Erasto Msuya kwenda kwa Miriam Mrita

Kibatala: Shahidi mimi nikifariki mke wangu anaweza kubadili umiliki wa gari TRA?

Shahidi: Ndio hapo sasa wote tufanye uchunguzi.

Kibatala: Ufanye uchunguzi na nani na wewe ndio umeleta hapa conclusion (hitimisho)? Wewe uliwahi kufanya uchunguzi TRA wa kubadilisha umiliki huo?

Shàhidi: Uchunguzi ulifanyika?

Kibatala: Ulifanya wewe?

Shahidi: Hapana

Kesi hiyo inaendelea tena Jumatatu katika hatua hiyo ya mahojiano ya dodoso baina ya mawakili wa utetezi na shahidi huyo na shahidi huyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live