Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kesi mauaji ya muuza madini kuendelea leo

Watuhumiwa Mtwara (600 X 590) Kesi mauaji ya muuza madini kuendelea leo

Mon, 27 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kesi ya mauaji ya mfanyabiashara wa madini, Mussa Hamis inayowakabili maofisa saba wa Jeshi la Polisi mkoani hapa inaendelea kunguruma leo baada ya kukwama kwa siku mbili mfululizo kwa sababu tofauti.

Kesi hiyo ya jinai namba 15 ya mwaka 2023 inayosikilizwa na Jaji Edwin Kakolaki kutoka Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, iko katika hatua ya usikilizwaji wa ushahidi wa upande wa mashtaka.

Leo Mahakama hiyo inatarajia kupokea ushahidi wa mashahidi kuanzia wa nane kati ya mashahidi 72 wanaotarajiwa kuitwa na kupande wa mashtaka; kadri muda utakavyoruhusu na kutegemeana na urefu wa ushahidi husika.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Mtwara (OC- CID), Mrakibu wa Polisi (SP), Gilbert Sostenes Kalanje; aliyekuwa Mkuu wa Kituo Kikuu cha Polisi (OCS) Mtwara na Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Charles Maurice Onyango.

Wengine ni aliyekuwa Ofisa Intelijensia ya Jinai Wilaya (DCIO) Mtwara ASP Nicholaus Stanslaus Kisinza; Mkaguzi Msaidizi Marco Mbuta Chigingozi; Mkaguzi John Yesse Msuya, aliyekuwa mganga mkuu wa Zahanati ya Polisi Mtwara na Mkaguzi Msaidizi, Shirazi Ally Mkupa na Koplo Salim Juma Mbalu.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na shtaka la mauaji wakidaiwa kumuua kwa maksudi Mussa Hamis katika Kituo cha Polisi Mitengo Wilaya ya Mtwara, Mkoa wa Mtwara, Januari 5, 2022 na kuutupa mwili wake Majengo, Kata ya Hiari karibu na kiwanda cha Sementi cha Dangote.

Jumatano Novemba 23 kesi hiyo ilikwama kusikilizwa baada ya mashahidi wote wawili wa upande wa mashtaka waliokuwa wameandaliwa kushindwa kufika mahakamani kutokana na kuugua.

Kiongozi wa jopo la waendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mkuu, Maternus Marandu aliieleza mahakama kuwa walikuwa wameandaa mashahidi wawili wa kutoa ushahidi siku hiyo lakini walipata changamoto za kiafya.

Alifafanua kuwa shahidi wa kwanza alipata changamoto ya afya tangu jana yake na wa pili vilevile alipata changamoto ya usiku wa kuamkia siku hiyo.

Hivyo aliiomba Mahakama ipokee ombi lao la ahirisho na iwapangie siku nyingine ya kuendelea na usikilizaji huo. Upande wa utetezi haukuwa na pingamizi kwa ombi hilo.

Kutokana na sababu hizo Jaji Kakolaki alikubaliana na hoja na ombi hilo la upande wa mashtaka na akaahirisha shauri hilo hadi siku iliyofuata (Alhamisi, Novemba 24), huku akiuwaelekeza upande wa mashtaka kuhakikisha unawapeleka mashahidi wake ili kesi hiyo iendelee.

Hata hivyo, Alhamisi ilipofika kesi hiyo haikuendelea, iliahirishwa hadi leo, baada Wakili Fredrick Ododa anayemwakilisha mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo, ASP Onyango, kufiwa na baba yake.

Jaji Kakolaki baada ya kupokea taarifa hiyo wa mdomo kutoka kwa wakili Emmanuel Dadaya kwa niaba ya kiongozi wa jopo la mawakili wa utetezi, Majura Magafu, alisema Mahakama ilikuwa imeshapokea pia kutoka kwa Wakili Ododa mapema asubuhi.

"....na kutokana na ukweli kwamba mshtakiwa wa pili anapaswa kuwa na uwakilishi wakati shauri linaendele, kwa misingi ya haki tunapaswa kuahirisha shauri hili ili mshtakiwa wa pili apate wakili atakayemwakilisha mpaka wakili wake atakapoungana nasi,” alisema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live