Dar Es Salaam. Hatimaye washtakiwa sita kwenye kesi ya mauaji ya aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk Sengondo Mvungi wamepewa Hakimu mwingine.
Hatua hiyo imetokana na washtakiwa hao kumkataa Hakimu wa awali, ambaye ni Hakimu Mwandamizi wa mahakaka hiyo, Augustina Mmbando aliyekuwa anaendesha kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Kwa sasa kesi hiyo yenye namba 6/2018 itasikilizwa, mbele ya Hakimu Mwandamizi, Augustine Rwizile wa Mahakama ya Kisutu.
Washtakiwa ni pamoja na Msigwa Matonya (35), Mianda Mlewa(45), Paulo Mdonondo (35), Longishu Losindo (34), Juma Kangungu (34) na John Mayunga (60), walipanda kizimbani jana Jumanne Juni 18,2019 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mbele ya Hakimu Mkazi Augustine Rwizile, wakati shauri hilo lilipopelekwa kwa kutajwa.
Washtakiwa walimkataa Hakimu Mmbando, wakidai kuwa hawana imani naye kwa madai kuwa haki yao inapotea.
Hakimu Mmbando alijiondoa kusikiliza kesi hiyo, Juni 4, 2019, wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa.
Pia Soma
- Wabunge wa CCM walalamikia Serikali kuchukua vyanzo vya halmashauri
- Naibu Waziri Mabula ahofia viwanda vya samaki kufa
- Waziri wa Madini wa Tanzania anguruma kwa dakika tano Paris
Hata hivyo jana, wakili wa Serikali Saada Mohamed aliieleza mahakama mbele ya Hakimu Mwandamizi, Augustine Rwizile kuwa jalada halisi la kesi hiyo bado hajalipata lilikuwa kwa Hakimu mwingine.
Saada baada ya kueleza hayo, Hakimu Rwizile alimtaka wakili huyo kuhakikisha analifuatilia kusudi tarehe ijayo awe na majibu ya kuifahamisha mahakama shauri lilipofikia.
Hakimu Rwizile aliahirisha kesi hiyo hadi Julai Mosi, 2019 itakapotajwa na washitakiwa walirudishwa rumande.
Katika kesi ya msingi, washitakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na shitaka la mauaji ambapo inadaiwa kuwa Novemba 3, mwaka 2013, walifanya kosa la mauaji ya kukusudia kinyume na kifungu cha 196 cha sheria na kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Ilidaiwa kuwa siku hiyo ya tukio, katika eneo la Msakuzi Kiswegere lililoko eneo la Wilaya ya Kinondoni, washitakiwa hao kwa pamoja walimuua kwa kukusudia Dk. Sengondo Mvungi ambaye mjumbe wa Katiba Mpya.