Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kesi mapenzi ya jinsia moja kuunguruma Septemba 10

14438 Pic+jinsi TanzaniaWeb

Wed, 29 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwanza. Ushahidi katika shauri linalowakabili watu wanne kwa kufanya vitendo vinavyoashiria mapenzi ya jinsia moja na makosa ya kimtandao, utatolewa siku mbili mfululizo.

Ushahidi huo wa upande wa mashtaka, utatolewa kati ya Septemba 10 na 11 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza.

Washtakiwa katika kesi hiyo namba 548/2017 ni Milembe Suleiman na Janeth Shonza, wanaodaiwa kuvishana pete ya uchumba licha ya kwamba wote ni wanawake. Wengine ni Aneth Mkuki anayeshtakiwa kwa kosa la kufanikisha sherehe hizo na Richard Fabian anayeshtakiwa kwa kosa la kusambaza video za sherehe hiyo.

Shauri hilo lilitajwa mahakamani hapo juzi kwa ajili ya mashahidi kutoa ushahidi, lakini ilishindikana baada ya wakili Jebra Kambole anayewatetea washtakiwa kutohudhuria mahakamani kwa madai ya kuwa na kesi nyingine jijini Dar es Salaam. Taarifa za Jebra zilitolewa na wakili Mwita Marwa ambaye aliiomba Mahakama kuipangia kesi hiyo tarehe nyingine kutokana na udhuru huo.

Upande wa mashtaka uliowakilishwa na wakili Emmanuel Luvinga, ulieleza kuwa kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kusikilizwa lakini baada ya wakili wa utetezi kutoa taarifa ya udhuru, hata wao hawakuleta mashahidi na kuomba kupangiwa tarehe nyingine.

Kutokana na hali hiyo, hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama ya mkoa anayesikiliza kesi hiyo, Rhoda Ngimilanga aliiahirisha na kupanga kuisikiliza kwa siku mbili mfululizo yaani Septemba 10 na 11 ili iishe.

Milembe na wenzake walifikishwa mahakamani hapo Desemba 8, 2017 huku hati ya mashtaka ikionyesha walitenda kosa hilo Agosti 31, 2017 katika Hoteli ya Pentagon jijini Mwanza.

Washtakiwa wote wapo nje kwa dhamana waliyoipata Desemba 15, 2017 baada ya kukamilisha masharti ya kila mmoja kuwa na mdhamini mmoja na kusaini hati yenye thamani ya Sh6 milioni.

Chanzo: mwananchi.co.tz