Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kesi kuingilia mawasiliano Airtel, taarifa za mtaalam wa mawasiliano zasubiriwa

44127 Pic+kesiii Kesi kuingilia mawasiliano Airtel, taarifa za mtaalam wa mawasiliano zasubiriwa

Wed, 27 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Upande wa mashtaka kesi ya kuingilia mfumo wa mawasiliano ya kampuni ya simu za mikononi ya Airtel, inayowakabili watu 11, wakiwemo wafanyakazi wa kampuni hiyo, umedai  unasubiri taarifa maalum za uchunguzi  kutoka kwa mtaalamu wa mawasiliano.

Mwanasheria wa Serikali,  Wankyo Simon ameeleza hayo leo Jumatano Februari 27, 2019 mbele ya Hakimu Mkazi mfawidhi, Kelvin Mhina, wakati shauri hilo lilipokuja kwa ajili ya kutajwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

"Washtakiwa wote wapo mbele ya mahakama yako na upelelezi wa shauri hili bado haujakamilika tunasubiri taarifa maalumu za uchunguzi  kutoka kwa mtaalam wa mawasiliano,  tunaomba terehe nyingine kwa ajili ya kutajwa" amedai Simon.

Hakimu Mhina baada ya kusikiliza maelezo hayo, ameahirisha kesi hiyo hadi Machi 26, 2019 itakapotajwa tena.

Washitakiwa katika kesi hiyo ni Erick Fidelis,  Zephania Maduhu, Anthony Masaki,  Lumuli Stanford, Ndeshiwonasiya Malle na Davis Waseda.

Wengine ni Goodluck Nyakira, Michael Onyango, Sylvester Onyango, Rodgers Laizer na Nancy Mwenda.

Katika kesi ya msingi washtakiwa hao wakabiliwa na makosa saba, likiwemo la kuingilia mfumo wa mawasiliano wa  Airtel bila ya kuwa na kibali.

Wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Septemba 9 na Desemba 24, 2018 jijini Dar es Salaam.

Katika shtaka la pili, siku na eneo hilo,  washtakiwa  huku wakijua kuwa ni kinyume cha sheria walijaribu kutenda kosa la wizi.

Kosa la  tatu,  Laizer na Nancy kwa makusudi na kinyume cha sheria,  wakiwa wafanyakazi wa Kampuni hiyo,  wanadaiwa walisababisha kuingilia mfumo wa mawasiliano ya Airtel bila ya kuwa na kibali.

Shtaka la nne, washtakiwa wote kwa pamoja  wanadaiwa kutoa taarifa za mfumo wa mawasiliano wa kampuni hiyo kinyume cha sheria.

Pia, Laizer na Nacy wanadaiwa kutoa taarifa ya mfumo wa mawasiliano ya  Airtel  kwa watu wasiohusika  na kampuni hiyo kinyume cha sheria.

Katika shtaka la sita inadaiwa washitakiwa hao waliingilia  mfumo wa mawasiliano wa kampuni hiyo bila ya kuwa na idhini. Katika shtaka la saba wanadaiwa  walipokea taarifa kupitia kompyuta bila idhini ya Airtel.

Washtakiwa wapo nje kwa dhamana.



Chanzo: mwananchi.co.tz