Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kesi Aveva, Kaburu kula Krismasi, Mwaka mpya lupango

32448 Hamaaa Tanzania Web Photo

Wed, 19 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Pamela Chilongola

Dar es Salaam. Kesi ya kughushi na kutakatisha fedha inayowakabili, vigogo wa klabu ya Simba, imeshindwa kuendelea na ushahidi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya mawakili wa utetezi wa mshtakiwa wa kwanza, Evans Aveva kushindwa kufika mahakamani hapo.

Mbali na Aveva ambaye ni rais wa zamani wa klabu hiyo, wengine ni Makamu wa wake,  Geofrey Nyange na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa Klabu ya Simba, Zacharia Hans Poppe.

Wakili wa Takukuru, Leonard Swai alidai leo mbele ya hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kuendelea na ushahidi.

"Shauri hili limekuja kwa ajili ya kuendelea na ushahidi na upande wa mashtaka tayari tuna mashahidi wawili na tuko tayari kuendelea," alidai Swai.

Swai baada ya kuelea hayo, wakili wa utetezi, Nestory Wandiba alisimama na kueleza mahakama kuwa mawakiki wawili wanaomtetea Aveva, wapo Mahakama Kuu.

"Mheshimiwa hakimu, mawakili Nehemia Nkoko na Wabea wapo Mahakama Kuu, wanakesi nyingine huko, hivyo tunaomba mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili yakuendelea na ushahidi" alidai Wandiba anayemtetea Nyange.

Hakimu Simba baada ya kusikiliza hoja za pande zote, aliwataka mawakili hao kuhakikisha wanafika mahakamani bila kukosa siku ambayo kesi hiyo itakapoendelea.

"Nataka mawakiki hawa wa utetezi kuhakikisha kuwa wanafika mahakami bila kikosa, Januari 3, 2019 wakati kesi hii itakapoendelea na ushahidi." alisema.

Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 3, 2019, itakapoendelea na ushahidi na washtakiwa Aveva na Nyange wamerudishwa rumande kutoka mashtaka yao kutokuwa na dhamana.

Tayari shahidi mmoja wa upande wa mashtaka ameshatoa ushahidi dhidi ya washtakiwa hao.

Shahidi huyo, Boaz Lubila (45), kutoka Benki ya CRDB makao makuu, alidai kuwaTaasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa iliandika barua kwa Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo wakiomba taarifa za miamala iliyofanywa katika akaunti tatu za Klabu hiyo.

Lubila ambaye aliajiriwa CRDB,  Oktoba 13, 1999,  katika Idara inayojihusisha na kusimamia shughuli za uendeshaji wa benki,  alidai kuwa Septemba 21, 2016,  Takukuru waliomba taarifa inayoonyesha miamala inayofanyika katika akaunti tatu za Klabu ya Simba.

"Katika akaunti hizo tatu walizoomba taarifa, muamala wa kwanza unaonyesha unaonyesha kutoa Dola 6000, wakati muamala wa pili ulikuwa ni kuhamisha Dola 300,000," alida Boaz.

Shahidi huyo alida kuwa Taasisi yoyote inayohitaji taarifa, lazima ipeleke barua kwa Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, ambaye yeye hatoa maelekezo kwa Mkurugenzi wa Idara husika.

Pia, alidai taarifa nyingine iliyoombwa na Takukuru ni nyaraka inayoonyesha miamala ya fedha inayotumwa katika akaunti (Swift message)

"Katika nyaraka hii ya Swift message, pia tuliombwa na nyaraka za fedha zinazotoka ambapo baada ya akuziprint, tuliziwasilisha Takukuru, Septemba 21, 2016," alidai shahidi huyo.

Kesi hiyo, inatokana na matumizi ya fedha za uhamisho wa mchezaji wa klabu hiyo, Emmanuel Okwi, kwenda Klabu ya Soka ya Etoile Sportive Du Sahel, ya Tunisia, kwa madai ya kutumia pesa hizo kununulia nyasi bandia na gharama za ujenzi wa uwanja huo.

Katika kesi hiyo Hans Poppe anakabiliwa na mashtaka mawili, ya kughushi nyaraka na kuwasilisha nyaraka za uwongo yeye pamoja na wenzake.

Aveva na Kaburu wanakabiliwa na mashtaka mengine zaidi ya matumizi mabaya ya madaraka kwa kuhamisha fedha hizo bila mamlaka ya Kamati ya Utendaji ya Simba, kujipatia pesa isivyo halali (Aveva) na utakayishaji fedha yanayowakabili wote, Aveva na Kaburu.

Washtakiwa Aveva na Nyange wanatetewa na mawakili Nehemia Nkoko na Nestory Wandiba wakati Hanspoppe yeye anatetewa wa Wakili Agostino Shio, Benedict Ishabakaki na Jebra Kambole.

Siku waliposomewa maelezo ya awali, washtakiwa hao wanadaiwa kuwa Machi 12, 2016,  Klabu ya Simba ililipwa jumla ya Dola za kimarekani 319, 212 na Klabu ya Etoile Sportive Du Sahel ya nchini Tunisia.

Kiasi hicho cha fedha kilikuwa ni ada ya uhamisho wa mchezaji Emmanuel Okwi kwenda Klabu ya Etoile Sportive Du Sahel ya nchini Tunisia.

"Fedha hizo ziliingizwa katika akaunti ya Klabu ya Simba kupitia akaunti namba O1J1026761800 iliyopo katika Benki ya CRDB tawi la Azikiwe.



Chanzo: mwananchi.co.tz