Amesema majalada takribani 50 ya ugaidi, yamekamilika na kwamba baadhi yake baada ya kupitiwa na kukosa ushahidi yamefutwa, huku waliofutiwa mashtaka wakipewa sharti la kuripoti vituo vya polisi walioko.
Aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam, baada ya kuzindua mafunzo ya mfumo wa kielektroniki uitwao ‘Case Management System, ambao utawezesha hati za mashtaka, kumbukumbu za kesi zinazosajiliwa polisi na kufikishwa mahakamani kuonekana papo hapo.
Mafunzo hayo ambayo yametolewa na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Mawasiliano na yanatolewa kwa waendesha mashtaka mawakili na maofisa polisi kutoka mikoa yote nchini kwa awamu tofauti.
Akifafanua zaidi, DPP alisema majalada hayo yakiwamo yalikuwa ya mauaji mashtaka yake yameshushwa kuwa mauaji bila kukusudia, kutokana na mengi yake ushahidi wake kushuka.
“Majalada ambayo tumeyapitia kwenye ofisi yangu kwa miezi sita, ni yaliyokamilika yataanza kupelekea mahakamani hivi karibuni baada ya mahakama kupanga usikilizaji. Majalada haya mengine ambayo mfano yapo 10 utakuta nane ndio yana ushahidi,” alisema Mwakitalu.
Akizungumza kuhusu mfumo huo ambao umeanza kutumika mkoani Mbeya, Mwanza na Arusha, DPP alisema sasa ofisi yake itaweza kufahamu majalada yaliyosajiliwa kila siku nchi nzima na kwamba itasaidia kuondoa mrundikano wa kesi.
Alisema kwamba changamoto kubwa iliyoko kwenye mahakama ni mrundikano wa kesi nyingi tangu mwaka 2000 kwa sababu ya kukosa upelelezi, alisema hivi sasa itakuwa rahisi kufahamu majalada yanayosajiliwa kila siku.
“Teknolojia inakua, hatunabudi kuwa na mfumo rafiki mahakamani. Kila mahakama, polisi itakuwa na kompyuta ingawaje si mara moja, ila zitakuwapo ili kufanikisha hili. Mfumo huu utaunganishwa polisi na mahakamani,” alisema DPP.
Wakili wa Serikali Mwandamizi Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Dodoma, Beatrice Mpembo, alisema, mfumo huo utarahisisha majukumu yao na kwamba vitendea kazi vikiwapo kila mahali itasaidia jukumu hilo kufanyika kila mkoa.
Mkaguzi wa Polisi, Mwendesha Mashtaka, Wilaya ya Kilwa, Juma Ndaile, alisema hivi sasa majalada yatakuwa hayamalizi saa 48 bila kusajiliwa kwenye mfumo huo.