Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kesi 23 rushwa ya ngono zafunguliwa

100255 Mahakama+pic Kesi 23 rushwa ya ngono zafunguliwa

Fri, 19 Jun 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), imefungua majalada 23 ya kesi za rushwa ya ngono, kumi kati ya hizo zikisikilizwa na tano kushinda katika mikoa mbalimbali.

TAKUKURU pia, imewataka wakuu wa vyuo kusimamia suala la rushwa ya ngono vyuoni ili kusaidia kupunguza ukandamizaji unaofanywa hususani kwa watoto wa kike.

Akizungumza na waandishi wa habari jana kwenye uzinduzi wa kampeni ya ‘Vunja ukimya kataa rushwa ya ngono’, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Brigedia Jenerali John Mbungo, alisema kila Mtanzania ana haki ya kutoa taarifa anapoona kuna viashiria vya rushwa ili izifanyie kazi na kutokomeza.

Alisema rushwa ya ngono ni tatizo kwa jamii na kazi yao ni kuisimamia na kuhakikisha wameitokomeza ili wanafunzi wasome kwa raha badala ya karaha kama ilivyo kwa wanafunzi wa kiume.

"Naomba watu tutumie huu mtandao wa vunja ukimya ili kusaidia kutoa taarifa, tunahitaji kuona kila mwanafunzi anakuwa na amani katika masomo yake," alisema Brigedia Jenerali Mbungo.

Kadhalika, alisema TAKUKURU, imejipanga kwa kushirikiana na Mfuko wa Wanawake nchini (WFT), kuhakikisha wanapiga vita hiyo rushwa ili wanafunzi waweze kusoma kwa amani na sio kukarahishwa na vitendo vya rushwa kila kukicha.

Alisema anawapongeza WFT, kutokana na kuonyesha ushirikiano mzuri wa kufanikisha kupinga vita rushwa ya ngono vyuoni.

Akizungumzia majalada yaliyofunguliwa ya kesi za rushwa alisema, yanaendelea kusikilizwa huku mengine yakionyesha kumalizika na kwamba watakuwa tayari wakati wowote kutoa msaada mtu anapokutana na vikwazo vya rushwa hususani kwa wanafunzi wa vyuo vikuu.

Hata hivyo, alisema kuna ripoti ya utafiti wa kisayansi ambazo zitasaidia kupata kila kitu kuhusu rushwa ya ngono, na huo ni mkakati ambao umewekwa katika taasisi za elimu.

Prof. Rukia Meena kutoka WFT, alisema mtizamo wa chuo utabadilika endapo wakuu wa vyuo watakuwa mstari wa mbele kupiga vita rushwa ya ngono ambayo imekuwa ikiwapasua vichwa wanafunzi.

Alisema wanafunzi wengi wanatoa malalamiko yao vyuoni na kuwataka wakuu wa vyuo kuwa mstari wa mbele kuwasikiliza na kuyafikisha sehemu husika ili yaweze kufanyiwa kazi na kutolewa uamuzi.

Alisema wanataka kuona wanafunzi wanasoma bila vikwazo vyovyote kutoka kwa wakufunzi wao jambo ambalo hivi sasa linapigiwa kelele.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live