Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kazi kuwadhibiti panya road imeanza

Kamanda Muliro Kazi kuwadhibiti panya road imeanza

Tue, 20 Sep 2022 Chanzo: Mwananchi

Baada ya matukio kadhaa ya uhalifu, Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam juzi lilitangaza kuwaua watu sita linalowatuhumu kuvamia nyumba, kujeruhi kwa mapanga hata kuua watu maarufu kama panya road.

Kamanda wa kanda hiyo, Jumanne Muliro alisema mauaji hayo yalifanywa Septemba 17, 2022 huko Makongo Area 4 ambapo wahalifu hao wakiwa kwenye gari aina ya Noah yenye namba za usajili T 260 DEP walikuwa njiani kuelekea Goba walikopanga kwenda kutenda uhalifu.

Muliro alisema walipata taarifa kisha kuwafuatilia na walipofika Makongo waliwakuta tisa na walipowaona askari wakawa wakataka kuwashambulia kwa mapanga ndipo polisi walipojibu mapigo na kuwaua sita kati yao.

Mwananchi lilienda eneo lilikotokea tukio hilo na kuzungumza na baadhi ya mashuda waliokiri kuwapo kwa mashambulizi.

Miriam Frank, mkazi wa Makongo Area 4 alisema “nilisikia milio ya risasi nikakimbilia chumbani kulala, sidhani kama walikuwa panya road, naamini ni majambazi kwa sababu vishindo vya risasi vilikuwa vikubwa.”

Shuhuda mwingine ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema tukio hilo lilitokea majira ya saa nne hadi saa tano usiku na hakukuwa na panya road bali majambazi.

“Wale ni majambazi, polisi wametunusuru na sijui walikuwa wanaenda kuvamia wapi, walikuwa na gari,” alisema shuhuda huyo.

Muuza duka lililo jirani na eneo lilipotokea tukio hilo aliyejitambulisha kwa jina la Tumsifu Eliya alisema alisikia milio ya risasi mara akawaona askari wawili wako jirani na duka lake, haraka akalifunga na kwenda kujificha.

“Tukio lile ni la ujambazi wala si watoto waliohusika, walikuwa na gari na kinachoonekana nao walikuwa na silaha pia walikuwa wanajibizana na polisi,” alisema.

Mkazi mwingine wa eneo hilo, Hawa Yahya alisema majibizano ya risasi yalitokea jirani kabisa na eneo analofanyia biashara.

“Muda mfupi tu baada ya kufunga biashara yangu, nikapigiwa simu majirani zangu wakiniuliza kama bado nipo, nikawauliza kwa nini wakaniambia polisi wanapigana risasi na majambazi. Nilipofika asubuhi walioshuhudia waliniambia polisi walisaidiana na wanajeshi ambao wako hapa jirani kuwapiga risasi majambazi,” alisema Hawa.

Alisema taarifa alizopewa na ndugu yake aliyempigia simu ni kuwa polisi walikuwa wanafukuzana na majambazi na walipofika eneo la Area 4, yakaanza majibizano ya risasi na wanajeshi waliposikia walitoka kuongeza nguvu kwa askari waliokuwapo.

Mkazi mwingine wa eneo hilo alisema gari la watuhumiwa lilipigwa risasi kwenye tairi.

“Wale majambazi walishuka wakajificha wakaanza kurushiana risasi wengine walikuwa wanajificha kwenye mitaro risasi zilipigwa mpaka tuliposikia kimyaa, wale majambazi wote walifia hapa, siku yao iliishia barabarani,” alisema shuhuda huyo.

Taarifa ya Polisi

Katika taarifa yake kwa waandishi wa habari jana, Kamanda Muliro alisema saa 4:15 usiku ya Septemba 17 katika eneo la Makongo Area 4, Jeshi la Polisi lilipata taarida fiche kutoka kwa raia wema kwamba wahalifu hao waliokuwa wanatokea Mabibo, walipanga kwenda kutekeleza uhalifu kwa kutumia mapanga eneo la Goba.

“Taarifa hizo tulizifuatilia kwa haraka na kikosi kazi kinachozuia vitendo hivi, ilipofika saa nne na robo eneo la Makongo Area 4 polisi walikutana na gari lililokuwa limebeba watuhumiwa hao wakiwa zaidi ya tisa, waliposimamishwa walisimama na kuelekezwa watoke ndani ya gari,” alisema kamanda huyo.

Hata hivyo, alisema watu hao walitoka garini wakiwa na mapanga huku wakitishia kuwajeruhi askari waliotaka wajisalimishe huku wakitaka kutoroka chini ya ulinzi jambo ambalo polisi waliwatahadharisha kwa kupiga risasi juu lakini walikaidi.

Katika mazingira hayo, alisema polisi walijihami na walifanya kila linalowezakana watuhumiwa hao waliokusudia kuwajeruhi wasiwatoroke.

“Katika purukushani hizo, watuhumiwa sita walijeruhiwa vibaya na watatu walifanikiwa kutoroka, majeruhi sita walipelekwa haraka hospitali ili wapate matibabu lakini kwa bahati mbaya walifariki dunia,” alisema kamanda huyo.

Alisema ndani ya gari la watuhumiwa hao walikuta mapanga sita na kisu kimoja na zana nyingine ambazo zimekuwa zikitumika kwenye uhalifu na panya road.

Kamanda Muliro alisema uchunguzi wa awali uliofanywa kwa watuhumiwa hao umebaini ni viongozi wa makundi ya unyang’anyi wa kutumia silaha na baadhi yao waliwahi kukamatwa na kufikishwa mahakamani kisha kuhukumiwa kifungo jela kwa tuhuma zinazofanana na hizi.

Aliwataja baadhi ya watuhumiwa hao kuwa ni Salum Juma Mkwama maarufu kama Babu Salum, mkazi wa Mbagala mwenye umri kati ya miaka 20 mpaka 27 na Khalifa mkazi wa Buguruni. Wote wawili waliwahi kushtakiwa kwa uhalifu wa mapanga.

“Vinara hawa wawili walishirika kwenye tukio la Septemba 14 lililotokea Kawe na Buguruni Ghana, watu kadhaaa walijeruhiwa na wengine kupoteza maisha,” alisema Muliro.

Hata hivyo, amewatahadhirisha wahalifu kuacha vitendo hivyo na wale watakaoendelea kukaidi watakamatwa kadiri mazingira yatakavyoruhusu.

“Jeshi la Polisi limesikia kilio cha wananchi na tutayafikia makundi yote kwa haraka na operesheni hii kali itaendelea,” alisema.

Mjadala taarifa ya polisi

Taarifa hiyo ya polisi imeibua mjadala mkubwa miongoni mwa wananchi wakihoji uhalali wa kutumia silaha za moto kwa wahalifu wasiokuwa na silaha za aina hiyo.

Hamis Ramadhani, mkazi wa Goba alisema kazi ya askari polisi si kuhukumu bali kuwakamata wahalifu na kuwafikisha mahakamani ili sheria ichukue mkondo.

“Ukisema unamuua jambazi si sahihi, huko ni kuishiwa mbinu. Kama mtu unamwona ni mhalifu jeshi lina mbinu, silaha ni njia ya mwisho kabisa, tena wakilazimika kutumia silaha ni kumjeruhi ili ajisalimishe na si kumuua,” alisema.

Mtaribu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumwa alisema kilichofanywa na polisi ni ukiukwaji wa haki za binadamu kwa kuwa watuhumiwa waliokuwa wakipambana nao hawakuwa na silaha za moto hivyo hakukuwa na sababu za wao kuzitumia silaha hizo.

Alisema taratibu za kipolisi ziko wazi kuhusu matumizi ya silaha za moto na huwa zinatumika pindi mtuhumiwa anapokuwa na silaha ya moto na anapoitumia kukabiliana na askari.

“Kama hawa vijana walikuwa na mapanga kama taarifa inavyoeleza basi polisi wangetakiwa kutafuta njia bora za kuwadhibiti sio kuwaua, jeshi la polisi halitakiwi kuua bali kuwakamata wahalifu na kuwapeleka kwenye vyombo vya sheria ili sheria ichukue mkondo wake,” alisema.

Akizungumzia hilo, Wakili Bashiru Yakub alisema kulingana na mazingira aliyoeleza Kamanda Muliro ni wazi polisi wamefanya mauaji yanayopaswa kuhojiwa.

Alisema askari wenye silaha wana mafunzo na mbinu ya kuzitumia silaha hizo hivyo hawakuwa na sababu ya kuzitumia kwa watu waliokuwa na mapanga.

“Haya ni mauaji kama mauaji mengine, mtu mwenye panga hawezi kumzidi nguvu askari mwenye silaha na mwenye mafunzo ya kuitumia hiyo silaha. Wangeweza hata kuwapiga kwenye miguu. Kama kweli walikuwa panya road hakukuwa na sababu ya kuwaua kwa sababu kupitia hao wangeweza kupata taarifa zaidi za mtandao wao,” alisema.

Kutoka mitandaoni

Hata hivyo, baadhi ya wananchi wamelipongeza Jeshi la Polisi wakisema panya roda limekuwa kundi tishio na kuzua hofu nchini.

“Safi kabisa! Panya road hawafai kupumua hapa Tanzania labda mbinguni kama Mungu atawasikiliza viumbe katili kama hawa, safi Polisi Tanzania” ameandika @mbwawa2 kwenye Instagram.

Naye Ritha Shivji, ameandika: “Jamani mkiwamaliza hao panya road mtakuwa mmefanya jambo kubwa sana maana wamekuwa tishio kwa jamii” wakati exavery838 akisema “hii sio issue ya kutangaza ni issue ya kudeal nao kimyakimya mpaka waishe. ukituhumiwa kuwa panya road unakula chako unazikwa maisha yanaendelea, wataisha tu mbona.”

“Kupitia mtandao wa Twitter, mbunge wa zamani wa Arusha Mjini, Godbless Lema aliandika “ni kama mafanikio dhidi ya uhalifu. Taarifa hii inapaswa kutazamwa kwa umakini. Naogopa tabia ya polisi ya kuchukua sheria mkononi.

Watu wasio na hatia wanaweza kuumizwa katika mkondo huu. Polisi wasio fuata maadili na sheria ni panya road walio vaa sare. Vilio mchanganyiko vitaibuka. Panya road ndani ya gari ya Noah walisimamishwa na polisi wenye SMG. Wakaamriwa kushuka katika gari. Wakatii amri lakini wakashuka na mapanga, ili wapambane na polisi? Ndipo Polisi wakawashambulia kwa risasi? Tupinge uhalifu kwa nguvu zote lakini kuhimiza sheria za nchi kufuatwa.”

Chanzo: Mwananchi