Dar es Salaam. Katibu wa CCM kata ya Kunduchi, Rashid Mchongea na mfanyabiashara Rose Mtuli wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni kwa makosa matatu likiwemo la kupokea rushwa ya Sh500,000.
Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Vera Ndeoya akisoma hati ya mashtaka leo Mei 21, 2019 mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Frenky Moshi, amedai washtakiwa hao wanakabiliwa na makosa ya kupokea na kutoa rushwa.
Ndeoya amedai kati ya Agosti Mosi na Agosti 15, 2018 Kunduchi, Mchongea aliomba hongo ya Sh500,000 kwa Rose kumshawishi ampunguzie kodi ya pango.
Katika shtaka la pili imeelezwa kuwa kati ya Agosti 15, 2018 katika eneo la Kunduchi, Mchongea alipokea hongo ya Sh500,000 kama kishawishi ili ampunguzie kodi ya pango.
Katika shtaka la tatu, kati ya Agosti 15, 2018 eneo la Kunduchi, Rose alitoa rushwa kwa Mchongea ili apunguziwe kodi ya pango.
Ndeoya amedai upelelezi upo kwenye hatua za mwisho na kuiomba mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya shauri hilo kutajwa huku washtakiwa hao wote wakikana mashtaka hayo.
Pia Soma
- Kesi ya 'Mpemba wa Magufuli ' kuanza kuunguruma kesho Kisutu
- Magufuli azipa miezi miwili taasisi kutoa gawio, zikishindwa...
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Mei 30, 2019 itakapotajwa tena.