Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kasoro za kisheria zamrejesha tena Kitilya, wenzake Kisutu

46140 Pic+kitilya Kasoro za kisheria zamrejesha tena Kitilya, wenzake Kisutu

Mon, 11 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar Es Salaam. Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, maarufu ‘Mahakama ya Mafisadi’ imewarejesha, Kamishna Mkuu mstaafu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya na wenzake wanne, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Uamuzi wa mahakama hiyo kuwarejesha katika Mahakama ya Kisutu, ulitolewa Machi 7, 2019 na Jaji Sirilius Matupa, baada ya kubaini kasoro katika mwenendo wa ufungaji na uhamishaji wa kesi hiyo kutoka Mahakama ya Kisutu kwenda Mahakama ya Mafisadi.

Kitilya na wenzake wanakabiliwa na mashtaka 58; ambapo mashtaka 49 kati ya hayo ni ya utakatishaji fedha, mashtaka matatu ya kughushi na mawili ya kutoa nyaraka za uwongo.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Miss Tanzania wa mwaka 1996, Shose Mori Sinare na Sioi Graham Solomon, ambao walikuwa maofisa wa Benki ya Stanbic.

Wengine ni aliyekuwa Kamishna wa Sera na Madeni Wizara ya Fedha, Bedason Shallanda (kwa sasa yuko Ofisi ya Waziri Mkuu) na Alfred Misana, ambaye alikuwa Kamishna Msaidizi wa Sera na Madeni kutoka wizara hiyo ambaye kwa sasa yuko wizara ya afya.

Kesi hiyo ilifungwa rasmi katika Mahakama ya Kisutu ilikofunguliwa awali kwa ajili ya kukamilisha taratibu za awali, Februari 12, 2019 na kuhamishiwa Mahakama ya Mafisadi, kwa ajili ya kuanza usikilizwaji kamili.

Hata hivyo leo Jumatatu Machi 11, 2019, washtakiwa hao wamerejeshwa tena Mahakama ya Kisutu, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, aliyeendesha mwenendo wa kesi hiyo awali, ili kurekebisha kasoro za kisheria zilizobainika baada ya kuhamishiwa Mahakama ya Mafisadi.

Mmoja wa mawakili wanaowatetea washtakiwa hao, Charles Alex, ameieleza mahakama kuwa jina la mshtakiwa wa tano lilisahaulika kuwekwa katika orodha ya washtakiwa wakati wa kuwasomea maelezo ya mashahidi na vielelezo (Committal Proceedings).

Hivyo aliomba jina hilo liingizwe kwenye orodha hiyo kama utaratibu wa kisheria unavyoeleza.

Katika kasoro nyingine, Wakili Alex amesema katika amri ya kuwahamishia washtakiwa hao kwenda mahakama yenye mamlaka ya usikilizaji wa kesi hiyo (Mahakama ya Mafisadi) haikuwataja washtakiwa wote kwa majina yao.

“Katika amri ya kuwahamishia washtakiwa hao kwenda Mahakama Kuu kitengo cha Mafisadi, kwa ajili usikilizaji wa kesi, haikuwataja washtakiwa wote kwa majina yao, badala yake ilitaja mshtakiwa wa kwanza na wenzake wanne” amedai Alex.

Alibainisha mahakama ilimtaja mshtakiwa wa kwanza tu kwa namba yake na kutumia neno wenzake, yaani mshtakiwa wa kwanza na wenzake, badala ya kuwataja kwa majina yao mmoja mmoja kama taratibu zinavyoelekeza.

Kutokanana maelezo hayo, Wakili wa Serikali Mkuu, Pendo Makondo ameieleza mahakama kuwa wako tayari kuanza kuwasomea upya washtakiwa hao maelezo ya mashahidi na vielelezo ili kurekebisha kasoro hizo, huku akitaja idadi ya mashahidi na vielelezo walivyonavyo.

Hata hivyo, mawakili wengine wa utetezi, Alex Mgongolwa na Majura Magafu wamepinga utaratibu huo wa kuanza upya kuwasomea maelezo ya mashahidi washtakiwa na vielelezo wakidai itachukua muda mrefu,

Badala yake wameshauri kwamba kwa kuwa tayari walishasomewa maelezo ya mashahidi na vielelezo hivyo basi yafanyike marekebisho kwa kuingiza majina ya washtakiwa hao kwenye orodha, ushauri ambao Hakimu Shaidi amekubaliana nao.

“Basi washtakiwa wote wataingizwa kwenye orodha kama kawaida,” amesema Hakimu Shaidi na washtakiwa wakarudishwa tena mahabusu.

Katike kesi hiyo Kitilya na wenzake wanadaiwa kutenda makosa hayo kwa nyakati tofauti tofauti kati ya Februari 2012 na Juni 2015 katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam na nje ya nchi.

Soma zaidi: Mahakama yawafutia kesi Kitillya na wenzake

Soma zaidi: Kitilya, wenzake wapandishwa upya kizimbani, wasomewa mashtaka 58



Chanzo: mwananchi.co.tz