Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kasoro hukumu ya kifungo cha maisha ilivyowaachia huru wafungwa wa ‘ubakaji’

24840 Pic+hukumu TanzaniaWeb

Wed, 31 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Baada ya kusota gerezani kwa miaka 15 wakitumikia kifungo cha maisha kwa kosa la ubakaji wa kikundi, hatimaye Mahakama ya Rufani imewarejesha uraiani wakazi wawili wa Mwanga mkoani Kilimanjaro, Richard Kimei na Emmanuel Kimaro baada ya kutengua adhabu hiyo.

Wameachiwa huru baada ya Serikali kuunga mkono rufaa yao kuwa Mahakama Kuu Moshi ilikosea kuwahukumu adhabu hiyo, huku mahakama ikisema upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha mashtaka dhidi yao.

Hukumu hiyo ilitolewa Oktoba 12 na jopo la majaji watatu, Bethuel Mmila, Richard Mziray na Mwanaisha Kwariko waliosikiliza rufaa hiyo mkoani Arusha.

Kwa mujibu wa hukumu hiyo ambayo Mwananchi imeiona, imesema Mahakama Kuu ilikosea kuwabadilishia kosa na adhabu kutoka adhabu ndogo waliyopewa kifungo cha miaka 30 kuwa kifungo cha maisha.

Awali, Kimei na Kimaro walihukumiwa na Mahakama ya Wilaya ya Mwanga, adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la ubakaji.

Walikata rufaa Mahakama Kuu lakini katika hukumu yake iliyotolewa Septemba 22, 2003 na Jaji Edward Rutakangwa, iliwabadilishia shtaka kutoka ubakaji na kuwa ubakaji wa kikundi (watu wengi kumbaka mwanamke kwa wakati mmoja) na ikawahukumu kifungo cha maisha jela.

Ndipo walipokata rufaa Mahakama ya Rufani wakiwasilisha hoja saba ambazo hata hivyo, mahakama iliziunganisha zikabaki tatu, moja ikisema wakati wa utambuzi wao kama watuhumiwa, hapakuwa na mazingira rafiki eneo la tukio na hivyo kutambuliwa kimakosa.

Pia, walikuwa wakidai kuwa Mahakama ya Wilaya na Mahakama Kuu zilikosea kuendelea kusikiliza na kuamua kesi yao bila kujali kwamba hati ya mashtaka ilikuwa na upungufu na kwamba, upande wa mashtaka haukuthibitisha mashtaka dhidi yao bila kuacha mashaka.

Siku ya usikilizwaji wa rufaa hiyo, warufani walijiwakilisha wenyewe bila kuwa na wakili, hivyo waliomba kwanza upande wa mjibu rufani uanze kutoa hoja zake kuhusu sababu zao za rufaa na kisha wao wafuatie.

Wakili wa Serikali, Fortunatus Muhalila alipinga hatia na adhabu hiyo ya kifungo cha maisha, kuwa haikuwa sahihi Mahakama Kuu kuwabadilishia shtaka kutoka shtaka dogo (ubakaji) kwenda shtaka kubwa (ubakaji wa kikundi).

Alidai kuwa kwa mujibu wa kanuni zinazotumika kwa makosa yenye asili moja mbadala hufanywa kutoka kosa kubwa kwenda kosa dogo na si kinyume chake.

Alisisitiza kuwa mahakama ilifanya mabadiliko hayo bila kuwapa warufani haki ya kujitetea kwa shtaka hilo jipya na ni kinyume cha kanuni za usikilizwaji wa haki na haki asili na hivyo kuliwaathiri warufani.

Hivyo, aliiomba mahakama hiyo itengue na kutupilia hatia na adhabu na kuwaachia huru warufani hao.

Kutokana na hoja hizo za Serikali, warufani hawakuwa na cha kuongeza badala yake waliomba Mahakama ya Rufani iwaachie huru.

Mahakama ya Rufani katika hukumu yake ilikubaliana na hoja za Serikali kisheria na kikanuni, huku ikisisitiza kuwa Mahakama Kuu ilichokifanya ni kinume cha kanuni na sheria.

Kutokana na kasoro hiyo mahakama kwa kutumia mamlaka yake ya kisheria ilitengua mwenendo na hukumu ya mahakama dhidi ya warufani.

“Kwa kawaida tungeamuru usikilizwaji wa rufaa Mahakama Kuu, lakini kwa kupitia kwa umakini ushahidi, tumebaini kuwa kesi dhidi ya washtakiwa haikuthibitishwa bila kuacha mashaka,” inasomeka hukumu hiyo na kusisitiza:

“Kutokana na ushahidi kutokutosha tunaona kwamba si vema kuamuru rufaa kuanza kusikilizwa upya. Kwa mazingira haya tunaamuru warufani kuachiwa huru mara moja isipokuwa tu kama wataendelea kushikiliwa vinginevyo kisheria.”

Chanzo: mwananchi.co.tz