Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kalemani aagiza Mkurugenzi akamatwe

C63c0852ce73b331231885fee61ccb88 Kalemani aagiza Mkurugenzi akamatwe

Mon, 17 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani ameagiza vyombo vya Ulinzi na Usalama kumkamata na kumuhoji Mkurugenzi wa kampuni ya NIPO kuhusiana na matumizi ya fedha za mradi wa kusambaza umeme katika vijiji 67 katika Wilaya ya Monduli mkoani Arusha.

Waziri Kalemani pia amewaagiza Mkurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), na Wakala wa Umeme vijijini (REA), kufuta mkataba wa kampuni hiyo.

“Naye Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni hii naye akamatwe wahojini na watueleze wapi wamepeleka fedha za Serikali kwa kuwa mradi umesimama kwa muda mrefu na fedha za umma zimetumika,"alisema.

Alitoa maagizo hayo juzi alipokagua utekelezaji wa mradi wa umeme katika Kijiji cha Lendikinya wilayani Monduli mkoani Arusha.

Kalemani pia alimuagiza Mkuu wa Wilaya ya Monduli Edward Balele kumtafuta na kumkamata na mwakalishi wa kampuni hiyo kwa kushindwa kukamilisha mradi kwa wakati.

"Mkuu wa Wilaya kamateni mwakilishi wa kampuni NIPO hawa ndio wanaikwamisha Serikali kutofikia malengo ya umeme kutofika vijijini kwa wakati''alisema.

Kalemani pia alimuagiza Meneja wa Tanesco, Mkoa wa Arusha, kumuondoa mhandisi aliyekuwa akisimamia mradi huo kuwa ameshindwa kuusimamia mradi ukamilike kwa wakati.

Alitoa siku 14, kwa mhandisi aliyeteuliwa kusimamia mradi huo, ahakikishe mradi unakamilika ndani ya muda na asipotekeleza hilo atamuondoa.

Aliwataka Mkurugenzi wa Tanesco na REA kuzingatia taratibu za manunuzi na kutoa tenda za miradi kwa wakandarasi wenye sifa na uwezo.

Aliwaagiza viongozi hao kukata asilimia 10 ya mshahara wa mkandarasi huyo kwa kuwa ameshindwa kutekeleza mradi kwa wakati, na kwamba fedha hizo zitumike kumlipa mkandarasi mpya.

Aliwataka wakurugenzi hao wahakikishe hadi mwishoni mwa Septemba mwaka huu, vijiji 67 vya Mkoa wa Kilimanjaro na vitano vya Wilaya ya Monduli mkoani Arusha, vinapata umeme.

Katika ziara hiyo, Kalemani aliambatana na viongozi wakuu kutoka Wizarani, akiwemo Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco na Mkurugenzi wa REA, pamoja na Mameneja wa Kanda ya Kaskazini wa shirika la umeme nchini.

Chanzo: habarileo.co.tz