Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kada CCM avamiwa, acharangwa mapanga Dar

74971 CCM+PIC

Mon, 9 Sep 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM) aliyekuwa mgombea ubunge wa Vunjo kupitia chama hicho mwaka 2015, Innocent Melleck amenusurika kifo baada ya kucharangwa mapanga na watu wasiojulikana jijini Dar es Salaam.

Melleck ambaye katika uchaguzi huo mwaka 2015 alichuana vikali na mbunge wa sasa wa jimbo hilo, James Mbatia (NCCR-Mageuzi) amecharangwa mapanga maeneo ya mwili eneo la kichwani, mabegani, mgongoni na kwenye mguu wa kushoto.

Akizungumza kwa taabu na Mwananchi leo Jumatatu Septemba 9,2019 amesema tukio hilo lilitokea usiku saa 5, Alhamisi iliyopita ya Septemba 5, 2019 akiwa jirani na nyumbani kwake Goba nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.

"Vijana wawili wakiwa na pikipiki walikuwa jirani na nyumbani kwangu, walionekana kama kuhitaji msaada, mmoja akasogea kwenye gari yangu akagonga," anasimulia.

Anasema alishusha kioo ili kumsikiliza, lakini kabla ya kuzungumza naye chochote alimfunika usoni na kitambaa na akapoteza fahamu.

"Sikujua kilichoendelea hadi nilipozinduka nikiwa hospitali ya Kairuki ambapo niliambiwa nilitupwa njia panda ya Kawe, nilisaidiwa na madereva bodaboda ambao walitoa taarifa Polisi Kawe," anasema

Pia Soma

Advertisement

Anasema waliomvamia walichukua fedha Sh11 milioni ambazo alikuwa nazo kwenye gari, flash mbili, laptop na simu mbili za mkononi.

 

"Nafikiri walikuwa na nia ya kuniua, kwani walinicharanga mapanga kichwani nikiwa nimepoteza fahamu, kwenye gari kulikuwa na vitu vingine vya thamani lakini hawakuchukua zaidi ya flash mbili, laptop, simu mbili za mkononi na fedha," anasema

Anasema tukio hilo limepeleka kuogopa kurejea nyumbani hata baada ya kuruhusiwa kutoka hospitali ambako amefanyiwa upasuaji mkubwa uliochukua saa nane.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Mussa Taibu alipoulizwa amesema wakati tukio linatokea alikuwa Shinyanga kikazi.

"Anayepaswa kunipa taarifa ni OCD ambaye nimejaribu kuwasiliana naye bahati mbaya yuko katika shughuli za mitihani," amesema Kamanda Taibu.

Mkuu wa Upelelezi Kawe, Alfred Lugamara amesema tukio hilo limeripotiwa polisi Kawe na upelelezi bado unaendelea.

"Mtu mmoja anaitwa Innocent Shirima (Melleck), kesi yake bado inachunguzwa, sababu mwenyewe hakuweza kutoa maelezo yoyote kutokana na hali yake kiafya, alichukuliwa Goba akatelekezwa njia panda ya kawe akiwa amejeruhiwa," alisema Alfred.

Chanzo: mwananchi.co.tz