Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kabendera bado anajadiliana na DPP

89047 Kabednerapic Kabendera bado anajadiliana na DPP

Wed, 18 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Upelelezi wa kesi ya uhujumu uchumi  inayomkabili mwandishi wa habari nchini Tanzania, Erick Kabendera bado haujakamilika.

Kabendera anakabiliwa na mashtaka matatu likiwemo la kutakatisha Sh173milioni katika Mahakama ya Hakimu ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Hayo yameelezwa leo Jumatano Desemba 18, 2019 na wakili wa Serikali mwandamizi, Wankyo Simon mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Janeth Mtega.

“Kesi ilikuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wake  bado unaendelea  tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa" amedai wakili Simon.

Baada ya Simon kueleza hayo, Jebra Kambole ambaye ni wakili wa Kabendera ameomba  upande wa mashtaka kukamilisha upelelezi kwa wakati ili kesi hiyo iweze kuendelea.

Amedai bado wanaendelea na mazungumzo na mkurugenzi wa mashtaka Tanzania (DPP) kuhusu barua ya kukiri na kuomba msamaha aliyoiandika Kabendera kwenda kwa DPP.

"Kesi hii ilivyoahirishwa wiki mbili zilizopita mahakama ilituambia tufuatilie kwa DPP kujua mazungumzo yamefikia hatua gani, naomba niseme tu tumeshafanya hivyo na mazungumzo bado yanaendelea" alidai Kambole na kuongeza

" Tutaifahamisha mahakama hii kadri mazungumzo yatakavyokuwa yanaendelea" amedai Kambole.

Hakimu Mtega baada ya kusikiliza hoja za pande zote ameahirisha kesi hiyo hadi Januari 2, 2020 itakapotajwa tena.

Mshtakiwa amerudishwa rumande kutokana na mashtaka yanayomkabili kutokuwa na dhamana.

Kabendera alifikishwa  Kisutu kwa mara ya kwanza Agosti 5, 2019 akikabiliwa na mashtaka matatu ambayo ni kuongoza genge la uhalifu, kukwepa kodi na kutakatisha zaidi ya Sh173.2 milioni.

Chanzo: mwananchi.co.tz