Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

#KESIYASABAYA: Shahidi adai Sabaya alimiliki genge la uhalifu

16795e4d1d4a1dcd5e733a68feb4449e.jpeg Lengai Ole Sabaya, aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai

Fri, 17 Dec 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Shahidi wa 13 katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya (34) na wenzake sita, amedai mahakamani kuwa Sabaya alikuwa akimiliki na kuratibu genge lililofanya uhalifu kwenye mikoa ya Arusha na Kilimanjaro.

Shahidi huyo, Ramadhani Juma (39) alidai hayo Alhamis wakati akiongozwa na mwendesha mashitaka mwandamizi wa serikali, Felix Kwetukia mbele ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha, Patricia Kisinda.

Juma alisema yeye alikuwa kiongozi mkuu wa kikosi kazi cha uchunguzi cha jalada la Sabaya akishirikisha maofisa wanane wakiwemo polisi. Shahidi huyo ni ofisa uchunguzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Arusha.

Alidai kuwa walikuwa wakichunguza jalada la tuhuma za rushwa ya shilingi milioni 90 zilizomkabili Sabaya na wenzake waliodaiwa kuchukua fedha hizo kwa mfanyabiashara, Francis Mrosso wa Arusha. Juma alidai kuwa Sabaya alimiliki wahalifu waliotumia silaha za moto na kwamba vijana alioshirikiana nao walikuwa na mafunzo ya kujilinda na pia walikuwa wakitumia majina bandia.

Alidai kuwa alikabidhiwa jalada Februari 22 mwaka huu na alipochunguza na kubaini kuwa alichunguza watu hatari alirudi kwa Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Arusha, James Ruge kuomba nguvu.

Juma aliieleza mahakama kuwa aliongezewa maofisa uchunguzi wanne wakiwemo wawili waliotoka makao makuu na wawili kutoka mkoani Kilimanjaro. Alidai kuwa waligundua kuwa wahusika kwenye genge hilo la uhalifu walitumia majina ya bandia akiwemo Sabaya aliyejiita Jenerali, mshitakiwa wa pili Enock Mnkeni (41) alikuwa akijiita Digidigi na mshitakiwa wa nne John Odemba alikuwa akijiita Night One.

Juma alidai kuwa mshitakiwa wa saba, Nathani Msuya (31) alikuwa akijiita Chersa, mshitakiwa mwingine ambaye hakuwepo mahakamani alikuwa akijiita Besigiye na mshitakiwa wa tano, Silverter Nyegu (26) alijiita Kicheche. Alidai kuwa walibaini kuwa watuhumiwa John Odemba na Daniel Mbura walikuwa wamekamatwa na walikuwa rumande polisi Arusha.

Juma alidai kuwa watuhumiwa walikiri kuhusika katika matukio ya kihalifu wakiwa na Sabaya na wengine ikiwemo la rushwa ya shilingi milioni 90, uporaji na unyang’anyi wa kutumia silaha katika duka la Shahiid Store lililopo Mtaa wa Bondeni jijini Arusha. Alidai kuwa kikosi cha kuwasaka Sabaya na wenzake kiliongezwa kwa kushirikisha polisi watatu wa Kituo Kikuu cha Polisi Arusha hivyo wakawa wanane.

Juma alidai kuwa walipata kibali cha kumtafuta Sabaya popote alipokuwa na uchunguzi wa awali ulibaini kijana huyo alijificha Dar es Salaam na kwamba kwa msaada wa kijana wa Moshi walimkamata usiku wa manane.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: